Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yanaendelea kupeleka misaada Sudan

Msaada wa chakula ukitolewa kwa jamii za Darfur Magharibi.
© WFP
Msaada wa chakula ukitolewa kwa jamii za Darfur Magharibi.

Mashirika ya UN yanaendelea kupeleka misaada Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imetoa taarifa hii leo ya juhudi za kibinadamu zinazoendelea nchini Sudan nchi ambayo inadumbukia katika vita tangu mwezi Aprili mwaka huu 2023. 

Taarifa kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa huko Darfur Magharibi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya watu, UNFPA limepeleka wafanyakazi wa afya na kijamii kusaidia maelfu ya wanawake na wasichana waliokimbia makazi yao na walio katika mazingira magumu na huduma za afya ya uzazi na ulinzi, ikiwa ni pamoja na kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.

Hapo jana huko mashariki mwa Sudan, UNFPA iliwasilisha vifaa vya kutosha vya afya ya uzazi ili kusaidia wanawake na wasichana 150,000 kwa muda wa miezi mitatu katika Hospitali ya Wazazi ya Port Sudan.

Katika Jimbo la Gedaref, timu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR zimekuwa zikisambaza msaada wa pesa taslimu kwa zaidi ya familia 830 za Sudan zilizolazimika kukimbia mzozo unaoendelea nchini mwao.

Katika Jimbo la White Nile, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF na wadau wake wamezindua kampeni ya kuokoa watoto. Takriban watoto 43,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wanapata chanjo ya surua, pamoja na Vitamini A na matibabu ya minyoo. 

Watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo mkali pia wanatibiwa mara baada ya kufanyiwa uchunguzi.