Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Agosti 19: Siku ya Kimataifa ya Watoa Misaada ya Kibinadamu

Bomu katika lori liliharibu makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad mnamo 19 Agosti 2003.
UN Photo/Timothy Sopp
Bomu katika lori liliharibu makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad mnamo 19 Agosti 2003.

Agosti 19: Siku ya Kimataifa ya Watoa Misaada ya Kibinadamu

Masuala ya UM

Siku ya Kimataifa ya Watoa Misaada ya Kibinadamu mwaka huu inaadhimisha miaka 20 tangu kutokea kwa shambulio baya kwenye Hoteli ya Canal mjini Baghdad, ndivyo anavyoanza ujumbe wake kwa ajili ya siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.  

Tarehe 19 Agosti 2003, shambulio la bomu kwenye Hoteli ya Canal huko Baghdad, Iraq, liliua wafanyakazi 22 wa misaada ya kibinadamu, akiwemo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Sergio Vieira de Mello. Miaka mitano baadaye, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la tarehe 19 Agosti kuwa Siku ya Kimataifa ya Watoa Misaada ya Kibinadamu (WHD).

“Siku hiyo ya giza, tulipoteza wenzetu 22, akiwemo Mwakilishi Maalum (wa Umoja wa Mataifa) Sergio Vieira de Mello.” Anasema Bwana Guterres. 

Msiba huo ulionesha badiliko katika jinsi wahudumu wa kibinadamu wanavyofanya kazi. 

Kwa sababu leo, ingawa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wanaheshimiwa ulimwenguni pote, wanaweza pia kulengwa na wale ambao wanaweza kuwadhuru.  

Mwaka huu, shughuli za kibinadamu duniani zinalenga kufikisha msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 250 katika nchi 69 ambayo ni mara kumi zaidi ya wakati ilipolipuliwa Hoteli ya Canal. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kwamba “ufadhili uko mbali sana. Migogoro inapoongezeka, haikubaliki kwamba wahudumu wa kibinadamu wanalazimishwa kupunguza misaada kwa mamilioni ya watu wanaohitaji.” 

Anazitaja changamoto zingine zilizoongezeka zaidi ya miaka ishirini iliyopita kuwa ni: 

Kuongezeka kwa mvutano wa kijiografia; 

Kupuuza waziwazi sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu. 

Kampeni za kushambulia na kutoa taarifa potofu kwa makusudi. 

Ubinadamu wenyewe sasa unashambuliwa. 

Lakini majaribio haya yameifanya jumuiya ya kimataifa ya kibinadamu kuwa imara zaidi. 

Wafanyakazi wahudumu wa misaada ya kibinadamu ambao wengi wao ni wafanyakazi wa kitaifa wanaofanya kazi katika nchi zao  wako karibu zaidi na watu wanaowahudumia. 

Wanatafuta njia mpya za kujitosa ndani zaidi katika maeneo yaliyokumbwa na maafa, na karibu na mstari wa mbele wa migogoro, inayoendeshwa na lengo moja: kuokoa na kulinda maisha. 

Guterres anapongeza akisema, “Katika Siku hii ya Kimataifa Watoa Misaada ya Kibinadamu, tunapongeza ujasiri na kujitolea kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu kila mahali.” 

Tunathibitisha tena uungaji mkono wetu kamili kwa juhudi zao madhubuti na za kuokoa maisha kote ulimwenguni. 

Tunasherehekea kujitolea kwao bila kuyumbayumba kuwahudumia watu WOTE wanaohitaji: 

“Haijalishi ni nani, haijalishi wapi; haijalishi ni nini.” Anahitimisha Guterres.