Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu watishia uhai wa watoto DRC – UNICEF

Amina Bakunda, Daktari katika kituo cha kutibu kipindupindu kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
© UNICEF/UNI407909/Benekire
Amina Bakunda, Daktari katika kituo cha kutibu kipindupindu kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu watishia uhai wa watoto DRC – UNICEF

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC linaonya kuwa kuimarika kwa mapigano mashariki mwa taifa hilo kumetumbukiza Watoto katika mlipuko mbaya Zaidi wa ugonjwa wa kipindupindu kuwahi kukumba taifa hilo katika kipindi cha miaka sita. 

UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC, inasema nchini kote, kumekuweko na wagonjwa 31,342 wa kipindupindu ambapo kati yao hao 230 wamekufa na hiyo ni kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu, wengi wao wakiwa ni watoto.

Jimbo lililoathirika zaidi ni Kivu Kaskazini ambako zaidi ya watoto 8,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano waliambukizwa kipindupindu katika miezi 7 ya mwanzoni mwa mwaka huu, idadi ambayo ni mara sita zaidi ya mwaka mzima wa 2022.

Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na wagonjwa 5,120 mwaka mzima wa 2022 ambako wagonjwa 1,200 walikuwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 5.

Hali ya sasa ni kengele ya dharura

"Ukubwa wa mlipuko wa kipindupindu na kiwango cha tishio lake vinapaswa kuwa kengele ya dharura,” amesema Shameza Abdulla, Mratibu wa dharura wa UNICEF Goma, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Amesema iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa ndani ya miezi ijayo, kuna hatari kubwa ugonjwa huo utasambaa maeneo mengine ya nchi ambayo hayashuhudia kipindupindu kwa miaka kadhaa.

Bi. Abdulla amesema kuna hatari pia kuwa kipindupindu kitaendelea kusambaa kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani ambayo tayari yana idadi kubwa ya watu hasa Watoto walio hatarini zaidi kuambukizwa magonjwa na hatimaye kifo.

Mwaka 2017 kipindupindu kilienea nchi zima ikiwemo mji mkuu wa DRC, Kinshasa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100 kati ya wagonjwa 55,000.

Vyoo vilivyojengwa na UNICEF na wadau wake katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo magharibi mwa mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/UNI418287/Ndebo
Vyoo vilivyojengwa na UNICEF na wadau wake katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo magharibi mwa mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Watu 159 wanatumia choo kimoja kambini DRC

UNICEF inasema kwa familia zinazoishi kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, uhaba mkubwa wa maji na huduma za kujisafi ni changamoto kubwa.

Takribani watu 300,000 wakiwemo Watoto 183,000 hawana maji ya kutosha, chini ya theluthi moja wana huduma za vyoo, ikimaanisha watu 159 wanatumia choo kimoja.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Wizara ya Afya ya Umma DRC kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu kwenye kaya zenye wagonjwa wa kipindupindu jimboni Kivu Kaskazini umebaini kuwa kati ya asilimia 62 hadi 99 ya kaya hizo ni familia ambazo mwaka jana zilifurushwa makwao.

Uchunguzi huo ulibaini pia familia kwenye maeneo yenye kipindupindu zina changamoto nyingine za kiafya ikiwemo utapiamlo na ukosefu wa huduma za wajawazito na chanjo.

UNICEF yahitaji dola milioni 62.5 kufanikisha operesheni zake

Sasa UNICEF inatoa wito wa dola milioni 62.5 ili kuimarisha harakati zake za kinga na operesheni dhidi ya kipindupindu sambamba na huduma za kujisafi kwa miezi mitano ijayo.

Fedha hizo zinalenga kufanikisha huduma hizo kwa watu milioni 1.8 wakiwemo watoto milioni 1.