Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupundu charejea na kasi mpya, chatishia uhai wa watu bilioni 1 duniani

Mtoto apewa chanjo ya kipindupindu huko Aleppo, kaskazini magharibi mwa Syria.
© UNICEF/Rami Nader
Mtoto apewa chanjo ya kipindupindu huko Aleppo, kaskazini magharibi mwa Syria.

Kipindupundu charejea na kasi mpya, chatishia uhai wa watu bilioni 1 duniani

Afya

Baada ya miaka mingi ya kupungua, gonjwa la kipindupindu sasa linarejea kwa kishindo likilenga nchi zilizo hatarini zaidi duniani, wameonya hii leo wataalamu wa afya wa Umoja wa Mataifa. 

Katika onyo hilo jipya, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO) na lile la kuhudumia watoto duniani (UNICEF) yanasema nchi nyingi zaidi hivi sasa zinakabiliwa na milipuko, huku idadi ya wagonjwa ikiripotiwa ikiwa ni kubwa kuliko miaka 10 iliyopita. 

Masikini wanakufa kwa kipindupindu 

“Janga la kipindupindu linaua maskini zaidi mbele ya macho yetu,” amesema Jérôme Pfaffmann Zambruni, Mkuu wa kitengo cha UNICEF kinachohusika na Dharura ya Afya Umma. 

Takwimu za WHO zinapigia chepuo mwelekeo huo wa kiza zikionesha kuwa hadi mwezi Mei mwaka jana, nchi 15 ziliripoti kuwa na wagonjwa wa kipindupindu, lakini hadi katikati ya mwezi huu wa Mei, “tayari tuna nchi 24 zinazoripoti kuwa na ugonjwa huo na tunatarajia idadi zaidi kutokana na kubadilika kwa majira,” amesema Henry Gray, Meneja wa WHO akihusika na hatua dhidi ya kipindupindu duniani. 

“Licha ya maendeleo yaliyopatikana miongo iliyopita katika mbinu za kudhibiti kipindupindu bado tuko hatarini kurudi nyuma.” 

WHO inakadiria kuwa watu bilioni moja katika nchi 43 wako hatarini kuuua kipindupindu huku watoto wenye umri wa chini ya miaka mitaon wakiwa hatarini zaidi. Kiwango kikubwa cha vifo kutokana na kipindupindu nacho kinatia hofu. Huko Malawi na Nigeria idadi ya vifo kutokana na kipindupindu ni kubwa ikifikia asilimia tatu mwaka huu, juu ya kiwango kinachokubalika cha asilimia moja. 

Yana Duka ni mmoja wa waathirika 35 wa cholera katika kituo cha afya cha muda mfupi kambini Muna nchini Nigeria. Alipoteza mimba yake baada ya kuwa mgonjwa. Picha: © UNFPA/Anne Wittenberg

Idadi ya wagonjwa wa kipindupindu inaongezeka 

Ukanda wa Kusini-mashariki kwa Afrika ndio umeathiriwa zaidi ambako maambukizi yanasambaa Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe. Mwenendo huu umekuja baada ya uharibifu uliofanywa na kimbunga Freddy mwezi Februari na Machi mwaka huu na kuacha watu 800,000 nchini Malawi na Msumbiji bila makazi yao huku huduma za afya zikiwa zimevurugika. 

Jamii hizi ziko hatarini kupata kipindupindu, gonjwa linalozuilika ambalo linashamiri kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa na mafuriko. 

Hali inakumba mbaya zaidi mvua kubwa na mafuriko vinapokutana na mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji duni kwenye sekta yam aji, huduma duni za kujisafi na usafi na kwingineko mapigano ya kivita, vitu ambavyo vinachochea kusambaa kwa magonjwa, yamesema mashirika hayo. 

Chanjo: mbinu lakini si jawabu kamilifu 

Ijapokuwa chanjo dhidi ya kipindupindu tayari inapatikana na inatumika, bado kiwango chake hakijakidhi mahitaji yanayoongezeka kila uchao. Kwa mujibu wa WHO, ombi la dozi milioni 18 za chanjo ya kipindupindu limekuwa likiwasilishwa kila mwaka lakini zinazopatikana ni chanzo milioni 8 pekee. 

Ongezeko la uzalishaji wa chanjo si suala la usiku mmoja,” anasema Bwana Gray akiongeza kuwa mpango ni kuongeza uzalishaji maradufu ifikapo mwaka 2025, « lakini hatutakuwa na dozi za kutosha iwapo mwelekeo wa sasa wa maambukizi utaendelea. Chanjo ni mbinu lakini sio jawabu kamilifu. Uwekezaji wa muda mrefu kwenye huduma za maji safi na kujisafi ndio kipaumbele.” 

Wito huo wa WHO umepaziwa sauti na UNICEF. “Sio tu tunahitaji uwekezaji wa muda mrefu, bali pia uwekezaji wa sasa hivi kwenye mifumo yam aji na kuhakikisha kila mtu anapata huduma ya majisafi na salama, huduma za kujisafi na za kiutu,” amesema Bwana Zambruni. 

Chanjo ya Cholera.(Picha:UM/JC McIlwaine)

Wito wa dharura kuwekeza kwenye maji 

Ili kukabili kitisho cha kipindupindu, WHO imezindua mpango wa kimkakati wa wa miezi 12  wa kujenga uwezo wa Kujiandaa, Kuchukua Hatua na Utayari  ukiwa na thamani ya dola milioni 160, sambamba na Wito kwa Hatua uliotolewa na UNICEF ukihitaji dola milioni 480. 

Mpango huo wa pamoja wa UNICEF na WHO utahusisha nchi 40 zilizo kwenye janga la kipindupindu. Hatua zitakazohusika ni uratibu, usimamizi wa maambukizi na kuzuia maambukizi pamoja na chanjo, matibabu, huduma za maji safi na salama na kujisafi. 

Bwana Gray amesema “ tunahitaij fedha ili kukamilisha mipango yetu.”