Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo mpya ya kipindupindu yaidhinishwa, ni ya matone

Mtoto mvulana akipokea chanjo ya kipindupindu nchini Haiti. (Maktaba))
© PAHO-WHO/David Spitz
Mtoto mvulana akipokea chanjo ya kipindupindu nchini Haiti. (Maktaba))

Chanjo mpya ya kipindupindu yaidhinishwa, ni ya matone

Afya

Muungano wa chanjo duniani Gavi na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hii leo wamekaribisha taarifa za kuidhinishwa kwa chanjo mpya ya kipindupindu iitwayo Euvichol-S ambayo ni ya matone na itapatikana duniani kote kwa bei nafuu. 

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya UNICEF imeeleza kuwa dawa hiyo ambayo ni muhimu sana katika mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu inatarajiwa kuanza kuzalishwa kwa kiasi kikubwa na bei nafuu na utasambazwa haraka ili kupambana na ongezeko kubwa la kimataifa la mlipuko wa kipindupindu. 

Pamoja na ukweli kuwa pikindupindu ni ugonjwa unaotibika lakini umekuwa ukigharimu maisha ya watoto wengi ulimwenguni ndio maana Mkurugenzi wa kitengo cha ugavi wa UNICEF Leila Pakkala  ameeleza kuwa wamefanikiwa kuagiza dozi zote zilizopo za chanjo hiyo na kwamba wataanza kuisambaza haraka iwezekanavyo.

“Idhini hiyo ina maana kwamba UNICEF inaweza kuongeza ununuzi na utoaji wa chanjo ya kipindupindu kwa zaidi ya asilimia 25, na hii itarudisha nyuma zaidi milipuko hatari ya kipindupindu.” Alisema Bi.Leila.

Uidhinishwaji wa chanjo hiyo ya matone ya kipindupindu unamaanisha utasaidia kuongeza usambazaji wa jumla wa chanjo ya kipindupindu ya kumeza inayopatikana mwaka wa 2024, na takriban dozi milioni 50 sasa zimetarajiwa  kupatikana ikilinganishwa na milioni 38 mwaka 2023.

“Kuidhinishwa kwa chanjo ya Euvichol-S kunawakilisha njia ya kuokoa maisha kwa jamii zilizo hatarini kote ulimwenguni,” amesema Dkt. Derrick Sim, Mkurugenzi Mkuu wa Masoko ya Chanjo na Usalama wa Afya wa Gavi.

Kipindupindu kimekuwa kikiongezeka duniani kote tangu mwaka 2021, huku kukiwa na viwango vya juu vya vifo licha ya kuwepo kwa matibabu rahisi, yenye ufanisi na nafuu. Idadi kubwa ya milipuko imesababisha mahitaji ya chanjo ambayo hayajawahi kutokea kwa nchi zilizoathiriwa.

Wadau wa masuala ya afya na nchi zilizoathirika na kipindupindu zimekuwa zikifanya kazi kwa dharura kusaka hatua za kukabiliana na kipindupindu, kuzuia na kudhibiti janga hili, na wametoa wito kwa nchi, wazalishaji na wengine kuunga mkono. 

Hivi karibuni, Gavi, UNICEF na wadau wengine walitangaza upelekaji mkubwa zaidi ulimwenguni wa uchunguzi wa kipindupindu lengo likiwa ni kusaidia kufanya uchunguzi na kupata majibu.

Soma hapa zaidi kuhusu taarifa hii.