Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baba yangu ndio kishawishi cha mimi kuwa msaidizi wa kibinadamu - Thomas Nyambane

Thomas Nyambane, Afisa wa usaidizi wa kibinadamu kutoka UNOCHA, akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu uzoefu wake wa utoaji wa misaada ya kibinadamu.
UN/Thelma Mwadzaya
Thomas Nyambane, Afisa wa usaidizi wa kibinadamu kutoka UNOCHA, akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu uzoefu wake wa utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Baba yangu ndio kishawishi cha mimi kuwa msaidizi wa kibinadamu - Thomas Nyambane

Msaada wa Kibinadamu

Siku ya watoa misaada ya kibinadamu huadhimishwa tarehe 19 ya mwezi Agosti kila mwaka kwa lengo la kutambua wale waliojitolea maisha yao kusaidia walio katika changamoto.Thomas Nyambane kutoka Kenya amekuwa mratibu wa misaada ya binadamu kwa zaidi ya miongo miwili na amehudumu kwenye mazingira magumu. 

Anaipenda kazi yake ila changamoto ni tishio la usalama na kila anapokuwa nje anaikumbuka sana familia yake kwani anapitwa na mengi. Hata hivyo, majukumu yake katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya binadamu na ile ya dharura, UNOCHA yanampa faraja kubwa kwani anapata nafasi ya kubadili maisha ya watu walio taabani.Mwandishi wetu wa Kenya, Thelma Mwadzaya alikutana naye mjini Nairobi alipokuwako kwa muda mfupi kabla kurejea Somalia ambako ndiko kituo chake cha kazi.

Tweet URL

1.Safari yako ilianzia wapi?

Baba yangu, hayati, nilipokuwa mtoto yeye ndiye naweza kusema aliyenipa motisha wa hii kazi ya kuwa na moyo wa kusaidia ama kufanya na mashirika yanayowasaidia wale ambao wameathiriwa na majanga mbalimbali na wanahitaji usaidizi. Pale utotoni, baba alikuwa mtu makini sana na taarifa za majanga yaliyotokea katika nchi za mbali na kuathiri watu ...kusababisha vifo na wengine kuwa wakimbizi wa ndani na nje.Nami nikavutiwa kutaka kujua hayo nikaanza kuyatilia maanani.Kwanza nilianza kufanya na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mambo ya makaazi-UN Centre for Human Settlement- ,halafu baadaye nikafanya na shirika la Msalaba Mwekundu-Red Cross, pamoja na serikali kisha nikarejea kwenye Afisi ya Umoja wa mataifa inayoratibu misaada ya binadamu na ya dharura, UNOCHA, ambako nimekuwa nikihudumu kwa miaka mingi ya zaidi ya 15.Muda mwingi nimehudumu Somalia, Sudan, Kenya na Pakistan.

2.Mnakopeleka huduma au ile misaada ya binadamu ni mazingira magumu na sasa huko mnasaidia nini?

Watu wengi walioathiriwa na majanga mbalimbali iwe ni vita, iwe ni matetemeko ya ardhi au mafuriko,wengi wao huwa wako katika hali ambayo hawawezi kujimudu.Hilo linawasukuma kuhitaji usaidizi kutoka nje na mara nyingi walioathirika duniani, ukichunguza wanatokea nchi masikini.Walioathirika pia wanatokea kwenye maeneo ambayo hayana uwezo zaidi.Hili ndilo linatufanya sisi kama wafanyakazi wa usaidizi wa binadamu tujitokeze kuzipa nguvu zaidi harakati zerikali zilizoathiriwa kuwa sasaidia wanyonge wasiojiweza baada ya hayo majanga kutokea. Kwa kweli,nchi nyingi zinazoathiriwa na haya majanga ndizo zilizo katika hali tete hivi kwamba pale tunapoenda kusaidia ni mazingira magumu. Kwengine hakupitiki kwasababu ya mafuriko,au hali ya anga sio nzuri kama hujaizowea au ni mahali palipo na vita.Unapata kuwa mahali tunapopeleka msaada pana vita au sisi wafanyakazi wa kutoa usaidizi wa binadamu tunalengwa na makundi ambayo hayataki kazi yetu ifanyike au watu wasaidiwe.

3.Misaada ya kibinadamu, ni kama ipi ?

Misaada ya binadamu tunayopeleka ni ile ambayo ni kwa walioathiriwa ili waendelee kuishi na kuokoa uhai.Mara nyingi inakuja kwa aina mbalimbali, kuna bidhaa za afya,chakula, vifaa vya kujengea makaazi au vyakula vya tayari mahsusi kwa watoto wachanga na kina mama.Mara nyingi wakati majanga yanatokea unapata ni kina mama na watoto wanaoathiriwa zaidi na msaada wa kibinadamu ndio njia pekee ya wao kuweza kuendelea kuishi.

Mama akimwangalia mwanae mwenye utapiamlo katika hospitali ya wilaya ya Luuq nchini Somalia.
UN Photo / Fardosa Hussein
Mama akimwangalia mwanae mwenye utapiamlo katika hospitali ya wilaya ya Luuq nchini Somalia.

4.Umetaja kwamba baadhi ya nyakati mnakofanyia kazi ni mazingira ya vita, usalama wenu uko hatarini. Sasa mnawezaje kutimiza majukumu yenu kuwasaidia walio na shida ?

Tunafanya kazi yetu kwa kufuata kanuni za kibinadamu zinazotuongoza ambazo ni kutoegemea upande wowote,kujitegemea,kuwa na ubinadamu na uadilifu.Kanuni hizo ndio muongozo wetu.Awali ziliheshimiwa sana hivi kwamba tunapopeleka misaada hatuwezi kuhujumiwa na mtu au kundi lolote.Lakini katika siku za hivi karibuni, makundi mengine yameanza kutoheshimu kanuni hizo na baadhi yetu kama wahudumu tunalengwa ima kwa hujma au kutekwa nyara na wakati mwengine kurushiwa makombora au kumiminiwa risasi na kuuawa.Hilo linahatarisha maisha ya baadhi ya wenzetu wanakofanyia kazi kuliko na shida kama hizo.

 

Ripoti hii imeandaliwa na Thelma Mwadzaya