Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubakaji na unyanyasaji wa kingono waongezeka Sudan

Mtaalamu wa UNICEF kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono akitoa elimu kwa watu waliokimbia makazi yao katika eneo la Wad Madani, mashariki ya kati mwa Sudan.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Mtaalamu wa UNICEF kuhusu unyanyasaji na ukatili wa kingono akitoa elimu kwa watu waliokimbia makazi yao katika eneo la Wad Madani, mashariki ya kati mwa Sudan.

Ubakaji na unyanyasaji wa kingono waongezeka Sudan

Amani na Usalama

Walaamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea kusikitishwa na ripoti za kuenea kwa vitendo vya ubakaji na ukatili wa kingono nchini Sudan unaodaiwa kutekelezwa na wanamgambo waasi wa kikundi cha Rapid Support Forces (RSF).

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka jijini Geneva Uswisi imewanukuu wataalamu hao wakieleza kuwa “Inadaiwa kuwa wanaume waliotambuliwa kama wanachama wa RSF wanatumia ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na wasichana kama zana ya kuiadhibu na kuitisha jamii.” 

Ripoti za wataalamu hao zinaonesha kuwa ikiwa ni miezi minne tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe iibuke nchini humo baadhi ya matukio ya ubakaji yanayoripotiwa yanaonekana kuwa ya kikabila.

Ushahidi pia umeonesha watetezi wanawake wa haki za binadamu walio ndani ya nchi hiyo pia wanalengwa moja kwa moja.

Vita hiyo nchini Sudan imeongeza changamoto za uhitaji wa kibinadamu ambapo maelfu ya raia wameuawa na mamilioni kuyakimbia makazi yao. Takriban wakimbizi 700,000 wameomba hifadhi katika nchi Jirani wameeleza wataalamu hao.

Sio wananchi wa Sudan pekee wanaoathirika na vita hiyo “Wanawake na wasichana wa Sudan katika maeneo ya mijini na vile vile huko Darfur wamekuwa hatarini kwa ukatili. Maisha na usalama wa wahamiaji na wakimbizi wanawake na wasichana, hasa kutoka nchini Eritrea na Sudan Kusini, pia yameathirika pakubwa.”

 

RSF na ukiukwaji wa haki za binadamu

Wataalamu hao walibainisha kuwa licha ya sera ya RSF kueleza hawatajihusisha na unyanyasaji wa kingono na kijinsia, lakini vitendo vingi vinavyoripotiwa vya kihalifu vinavyoripotiwa mara kwa mara vinahusishwa kutekelezwa na RSF.

Huku wakitoa wito kwa pande zote zinazogombana kukomesha ukiukwaji wa sheria za kibinadamu na haki za binadamu, wataalam hao walielezea wasiwasi wao mahususi kutokana na ripoti thabiti za ukiukwaji mkubwa unaofanywa na RSF, zikiwemo ripoti kwamba wanawake na wasichana wametoweshwa na vitendo, kulazimishwa kufanya kazi, na unyonyaji kingono.

Imeripotiwa kuwa mamia ya wanawake wamezuiliwa na RSF, wakiwa katika mazingira ya kinyama au ya kudhalilishwa, kushambuliwa kingono, na wako katika hatari ya utumwa wa ngono.

Ufikishaji wa misaada kwa waathirika unatatizwa na mapigano yanayoendelea nchini Sudan ambapo inakuwa vigumu kwa wataalamu kuwafikisha huduma hizo muhimu Pamoja na huduma nyingine kama za afya ya uzazi.

 RSF wametakiwa kuonesha dhamira yake ya kweli ya kuzingatia wajibu wa kibinadamu na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kuzuia unyanyasaji wa kijinsia na kuruhusu usafirishaji wa misaada ya kibinadamu na kuwawajibisha wale wote wanaotenda vitendo viovu.