Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni changamoto ya haki za binadamu duniani-Guterres 

25 Novemba 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kwa siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake inayoadhimishwa kila Novemba 25, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kwani ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni changamoto ya haki za binadamu ulimwenguni.

Bwana Guterres amesema janga la COVID-19 limedhihirisha zaidi suala hili la ukatili dhidi ya wanawake kama dharura ya ulimwengu inayohitaji hatua za haraka katika ngazi zote, katika nafasi zote na watu wote na kwamba anguko la kijamii na kiuchumi kutoka kwa janga hili kunawasukuma wanawake na wasichana katika umaskini, na hatari ya unyanyasaji dhidi yao inaongezeka. 

Katibu huyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “mwezi Aprili mwaka huu, nilihimiza jamii ya kimataifa ifanye kazi kumaliza janga kivuli la unyanyasaji wa kijinsia mara moja na milele. Narudia tena na kuzindua tena ombi hilo leo.” 

Aidha Bwana Guterres amesisitiza kuwa, jamii ya ulimwengu inahitaji kusikia sauti na uzoefu wa wanawake na wasichana na kuzingatia mahitaji yao, hasa manusura na wale ambao wanakabiliwa na aina nyingi na mtambuka za ubaguzi. “Lazima pia tupatie kipaumbele uongozi wa wanawake katika kutafuta suluhisho na kushirikisha wanaume katika mapambano.” Ameeleza.  

Vilevile Bwana Guterres amesema hatua lazima ihusishe ufadhili wa kutabirika na rahisi kwa mashirika ya haki za wanawake, ambao mara nyingi ndio huchukua hatua ya kwanza wakati wa mizozo n ani muhimu kwamba huduma kwa manusura wa ghasia zibaki wazi, na rasilimali na hatua za kutosha kusaidia majibu ya kiafya, kijamii na haki. 

 “Hatua hizi hazipaswi kuzingatia tu kuingilia kati mara tu unyanyasaji wa wanawake unapotokea. Wanapaswa kufanya kazi kuzuia unyanyasaji kutokea kwanza, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kanuni za kijamii na ukosefu wa usawa wa nguvu, na polisi na mifumo ya kisheria inahitaji kuongeza uwajibikaji kwa wahalifu na kumaliza kulindwa kwa watenda uovu.” Amesisitiza Guterres.  

Bwana Guterres amehitimisha kwa kusema katika siku hii ya kimataifa, "tuongeze juhudi zetu za kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia milele." 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter