Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za unyonyeshaji mtoto pahala pa kazi zimeanza ‘kulipa’ -UNICEF/WHO

Mundene, mama nchini Ethiopia akiwa makini katika kumnyonyesha mwanaye hadi atimize umri wa miezi 6
Picha na UNICEF/Ayene
Mundene, mama nchini Ethiopia akiwa makini katika kumnyonyesha mwanaye hadi atimize umri wa miezi 6

Sera za unyonyeshaji mtoto pahala pa kazi zimeanza ‘kulipa’ -UNICEF/WHO

Afya

Ikiwa leo ni mwanzo wa Wiki ya Kimataifa ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama kwa mtoto, kaulimbiu ikiwa, "Tufanye unyonyeshaji kazini, ufanye kazi" Mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) na la Afya Ulimwenginu (WHO) wanasisitiza haja ya usaidizi mkubwa wa unyonyeshaji katika sehemu zote za kazi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wakuu wa mashirika hayo Catherine Russell wa UNICEF na Dkt. Tedros Ghebreyesus wa WHO hii leo huko Geneva, Uswisi na New York, Marekani inasema hatua hiyo ni muhimu ili kuendeleza na kuboresha maendeleo katika viwango vya unyonyeshaji duniani kote huku ushauri wao ukijumuisha likizo ya uzazi yenye malipo ikiwezekana kwa muda wa miezi sita au zaidi baada ya kujifungua. 

Somalia nayo imo kwenye nchi zilizopata maendeleo

“Katika miaka 10, nchi nyingi zimefikia maendeleo makubwa ya kuongeza viwango vya akina mama kunyonyesha Watoto wao. Ingawa hivyo maendeleo makubwa zaidi yanawezekana pindi hatua za akinamama kunyonyesha Watoto zinalindwa na kupata usaidizi hasa pahala pa kazi,” imesema taarifa hiyo.

Ongezeko limekuwa kwa takribani asilimia 10 hadi kufikia asilimia 48 ambapo nchi kama Cote d’Ivoire, visiwa vya Marshall, Ufilipino, Somalia na Vietnam zimepata ongezeko kubwa na kudhihirisha kuwa maendeleo yanaweza kuweko pindi unyonyeshaji mtoto kutoka kwa mama unalindwa na kusaidiwa.

Mama kusini mwa Malawi akimyonyesha mwanae wa kike mwenye umri wa miezi 6.
© UNICEF/Thoko Chikondi
Mama kusini mwa Malawi akimyonyesha mwanae wa kike mwenye umri wa miezi 6.

Hatua zaidi zahitajika kufikia lengo 2030

Hata hivyo taarifa hiyo inasema kufikia lengo la dunia la asilimia 70 ifikapo mwaka 2030 kutahitaji kuondolewa kwa vikwazo ambavyo wanawake na familia wanakumbana nazo wakati wa kunyonyesha Watoto maziwa ya mama.

Mathalani usaidizi pahala pa kazi. Ushahidi unaonesha kuwa wakati kiwango cha mama kunyonyesha mtoto wake maziwa yake anapoanza kazi kinapungua, hatua hiyo inaweza kubadilishwa iwapo maeneo ya kazi yatakuwa na sehemu ya mama kuweza kuendelea kunyonyesha hata akirejea kazini.

Sera zingine kama vile likizo ya uzazi ya malipo, muda wa mapumziko wakati wa kazi ili mama anyonyeshe mtoto na vyumba ambavyo mama anaweza Kwenda kunyonyeshea mwanawe wakati wa kazi au Kwenda kupampu maziwa na kuyahifadhi, zinaweza kusaidia.

Sera za uwezeshaji mama kunyonyesha mtoto zina faida kiuchumi

WHO na UNICEF wanasema sera hizi zina mafanikio kiuchumi kwa sababu zinapunguza kiwango cha mwanamke kutokuweko kazini kwa ajili ya kunyonyesha mtoto, kunaongeza kiwango cha kushikilia wafanyakazi wanawake na kupunguza gharama za kuajiri na kufundisha wafanyakazi wapya pindi wanawake wanaojifungua wanapoacha kazi kwa ajili ya kulea Watoto wao.

Kuanzia nyakati za mwanzoni za uhai wa mtoto, unyonyehaji maziwa ya mama ni hatua muhimu ya kulinda uhai na maendeleo ya mtoto, imesema taarifa hiyo.

Unyonyeshaji mtoto maziwa yamama humlinda dhidi ya magonjwa ambukizi na kuongeza kiwango cha kinga ya mwili yam toto.

Watoto ambao hawanyonyeshwi maziwa ya mama wako mara 14 zaidi hatarini kufariki duia kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja kuliko wale ambao wamepatiwa maziwa ya mama yao.

Mhudumu wa afya Moldova akisamidia mama anyonyeshae kumnyonyesha vizuri mtoto wake
© UNICEF/Tapes Ion
Mhudumu wa afya Moldova akisamidia mama anyonyeshae kumnyonyesha vizuri mtoto wake

Nini kifanyike? Mambo makuu matatu

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF na WHO wanataka serikali, wahisani, jamii, sekta binafsi kuimarisha hatua zao kusaidia mazingira bora ya mama kunyonyesha mtoto pahala pa kazi; iwe sekta rasmi au isiyo rasmi.

Kupatia wanawake na walezi wanaofanya kazi, likizo ya uzazi ya malipo ili wakidhi mahitaji ya Watoto wao.  Hii ni angalau wiki 18 za likizo ya uzazi ya malipo, hasa miezi sita baada ya kujifungua.

Mashirika hayo pia yanataka uwekezaj katika sera za usaidizi wa programu za akina mama kunyonyesha Watoto wao katika mazingira yoyote.