Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo vya Habari Afghanistan havitoi taarifa: Wataalamu wa UN

Kundi la wanawake na watoto wao wakitembea Daikundi katika eneo la mbali la katikati mwa Afghanistan.
© UNICEF/Mark Naftalin
Kundi la wanawake na watoto wao wakitembea Daikundi katika eneo la mbali la katikati mwa Afghanistan.

Vyombo vya Habari Afghanistan havitoi taarifa: Wataalamu wa UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa hii leo wameelezea wasiwasi wao kufuatia vyombo vya habari nchini Afghanistan kutotoa taarifa ya tukio la Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa ambalo lilizungumzia haki za wanawake na wasichana nchini humo mnano mwezi Juni 2023.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa jijini Geneva Uswisi umewanukuu wataalamu hao wakieleza kuhuzunishwa na waandishi kutotoa taarifa kwa umma wakieleza kuwa matukio kama hayo ndio sehemu salama kwa wanawake kupaza sauti zao na kutoa maoni yao.

Jambo jingine lililowahuzunisha ni baadhi ya walioshiriki katika tukio hilo wameanza kusambaziwa taarifa za kuwachafua.

“Tumesikitishwa na chombo cha habari kinachoitwa Afghanistan International ambacho kimechagua kutumia vibaya mjadala huo muhimu kuhusu haki za wanawake na wasichana wa Afghanistan katika Baraza la Haki za Kibinadamu na kuanzisha kampeni ya kashfa dhidi ya mzungumzaji mmoja mwanamke wa Afghanistan aliyealikwa pamoja na mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa.” Wamesema wataalamu hao.

Wataalamu hao wametoa wito kwa jamii yote kuzingatia, kurejesha na kulinda haki za binadamu za wanawake na wasichana nchini Afghanistan, ikiwa ni pamoja na kuheshimu maoni mbalimbali, hasa yale yanayoshikiliwa na kupigiwa chepuo na wanawake wenyewe.

Ingawa ukosoaji wa wazungumzaji kwa misimamo wanayochukua kuhusu masuala ya haki za binadamu inakubalika, washiriki wote wanapaswa kuwa huru na kutopokea vitisho, unyanyasaji, au aina nyinginezo za kulipiza kisasi. 

“Mashambulizi ya kibinafsi, kuingiliwa kwa faragha, na kueneza habari potofu za kijinsia kunaweza kuwa na athari mbaya kwa ulinzi na usalama wa watu walioathiriwa na kuharibu sifa zao.” 

Wataalamu hao wamehitimisha taarifa yao kwa kueleza kuwa si vyema kumtupia lawama mfanyakazi wa UN kwani wenye mamlaka husika na wafanyakazi wakuu wa Umoja wa Mataifa, bila kumjumuisha mfanyakazi aliyetambuliwa na anayeshambuliwa ndio walihusika na uratibu wa tukio hilo, kuchagua na kuwaalika wazungumzaji katika tukio hilo kulingana na utaratibu uliowekwa, wakiweka kipaumbele kwa wingi wa sauti na maoni yanayohusiana na mada husika zilizowasiliahwa.