Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya watu duniani hatarini kuugua Dengue: WHO

Jamaa wakisubiri nje ya hospitali moja huko Kassala, Sudan, ambapo dada yao mwenye umri wa miaka 28 anatibiwa homa ya dengue. (Maktaba)
OCHA/Saviano Abreu
Jamaa wakisubiri nje ya hospitali moja huko Kassala, Sudan, ambapo dada yao mwenye umri wa miaka 28 anatibiwa homa ya dengue. (Maktaba)

Nusu ya watu duniani hatarini kuugua Dengue: WHO

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limesema takriban nusu ya idadi ya watu ulimwenguni hivi sasa wapo hatarini kuungua ugonjwa wa Dengue huku ikikadiriwa kila mwaka watu kati ya milioni 100 mpaka 400 wanapata maambukizi.

Dengue ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes. Ugonjwa huo hutokea zaidi katika nchi zenye hali ya hewa ya kitropiki na ya joto. 

Mkuu wa Kitengo kinachohusika na magonjwa ya Kitropiki yasiyopewa kipaumbele ambaye pia ni mratibu wa mpango wa magonjwa ya Dengue na Arbovirus katika shirika la Afya ulimwenguni WHO Dkt. Raman Velayudhan, akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi amesema ugonjwa huu wa Dengue “Umeongezeka kwa kasi duniani kote katika miongo ya hivi karibuni, huku idadi ya wagonjwa wanaoripotiwa WHO wakiongezeka kutoka nusu milioni mwaka 2000 hadi zaidi ya milioni 4.2 mwaka 2022. Hiyo ni takriban mara 8 zaidi katika miongo miwili."

Ugonjwa wa Dengue, ambao pia huitwa homa ya mfupa, ni maambukizi ya kawaida ya virusi ambayo huenea kutoka kwa mbu hadi kwa binadamu. Watu wengi walio na ugonjwa huu hawana dalili na hupata nafuu baada ya wiki 1 mpaka 2. 

Hata hivyo Dkt. Velayudhan amesema “Kwa wengine hupata dalili za kawaida ikiwemo homa kali, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, kichefuchefu na vipele. Iwapo mtu ataugua na kupona na kisha kuugua kwa mara ya pili ana uwezekano mkubwa kupata dalili za dengue kali.”

Watu ambao hupata Dengue kali wanahitaji kupatiwa matibabu hospitalini kwani wakichelewa wanaweza kupoteza maisha.

Ingawa hakuna matibabu kamili ya ugonjwa huu mpaka sasa , wale wanaogundulika hupatiwa dawa za kupunguza joto na maumivu ya mwili.

Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya
IAEA
Mbu aina ya aedes aegypti ambaye anaeneza ugonjwa wa zika, bila kusahau dengue na chikungunya

Watu wanaweza kupunguza hatari ya kupata dengue kwa kuepuka kuumwa na mbu, hasa mchana.

Wakati takriban asilimia 70 ya wagonjwa wengi wakiripotiwa kutoka Barani Asia, Ukanda wq Jangwa la Sahara idadi kubwa ya wagonjwa wameripotiwa kutoka nchini Sudan ambapo kulikuwa na wagonjwa 8239 na vifo 45 tangu Julai 2022. 

Katika wiki za hivi karibuni WHO imepokea ripoti za uwepo wa wagonjwa wa dengue nchini Misri.

WHO imezitaka wizara za Afya kuchukua hatua kwani wakati kuna milipuko, dengue inaweza kuchukua rasilimali za thamani kutoka kwenye mfumo wa afya, na kuongeza mzigo zaidi kwa taifa.