Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nelson Mandela alikuwa shujaa wa ujasiri na amani, tumuenzi kwa vitendo: Guterres

Nelson Mandela akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa September 2004 (Kutoka Maktaba)
UN Photo
Nelson Mandela akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa September 2004 (Kutoka Maktaba)

Nelson Mandela alikuwa shujaa wa ujasiri na amani, tumuenzi kwa vitendo: Guterres

Haki za binadamu

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika sherehe za maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Mandela ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amewataka watu kuenzi maisha na urithi wake kwa kukumbatia roho yake ya ubinadamu, utu na haki.

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akitoa hotuba yake katika sherehe za kila mwaka za kukumbuka maisha na urithi wa Nelson Mandela.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akitoa hotuba yake katika sherehe za kila mwaka za kukumbuka maisha na urithi wa Nelson Mandela.

Guterres amesema “ Nelson Mandela alikuwa shujaa wa ujasiri na imani, kiongozi wa mafanikio makubwa na ubinadamu wa kipekee, jabalí la wakati wetu ambaye urithi wake tunauheshimu zaidi kupitia vitendo kwa hatua ya kufukuza sumu ya ubaguzi wa rangi, ubaguzi na chuki. Hatua za kuzima urithi wa ukoloni na hatua ya kukuza usawa, haki za binadamu na zaidi ya yote haki.”

Katibu Mkuu amesema leo hii umasikini, njaa na kutokuwepo kwa usawa vinaongezeka huku mataifa yakizama kwenye lindi la madeni.

Pia amesema changamoto zingine kama mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unasambaratisha maisha ya wale wasio huika kabisa na kuusababisha mgogoro huo.

Kana kwamba hayo hayatoshi Guterres amesema “na mfumo wetu wa kifedha wa kimataifa usio wa haki na uliopitwa na wakati hautekelezi kazi yake kama chombo cha hifadhi salama ya jamii duniani.”

Pamoja na hayo amesema ndani ya uwezo wetu dunia inaweza kutatua kila moja ya changamoto hizi.

Kwa hivyo ametoa wito, “Hebu tusimame na wanawake na wasichana, vijana na waleta mabadiliko kila mahali na tuchukue hatua kujenga ulimwengu bora.”

Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zimekuwa msitari wa mbele kuzisaidia nchi katika masuala ya haki zikiwemo za mawafungwa
MINUSCA/Leonel Grothe
Operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa zimekuwa msitari wa mbele kuzisaidia nchi katika masuala ya haki zikiwemo za mawafungwa

Wafungwa ni sehemu ya jamii

Kampeni ya siku ya Mandela mwaka huu 2023 inamulika haki kwa wafungwa ikipewa jina #PrisonersMatter.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa na uhalifu UNODC inaeleza ni kwa nini wafungwa nao wanastahili na umuhimu wa kampeni hiyo, huku ikitoa wito kwa dunia kutumizi kiutendaji kanuni za kiwango cha chini cha Umoja wa Mataifa kwa za jinsi ya kuwatendea wafungwa , kanuni za Nelson Mandela.

Ofisi hiyo imesema “Wafungwa mara nyingi ni watu waliosahaulika, wengi wanawafikiria kuwa wamejitenga na jamii nzima, wameondolewa kama adhabu ya jinai au wakisubiri kesi. Lakini wafungwa hawajajitenga nasi. Ni zao la jamii na watabaki kuwa sehemu ya jamii zetu, na idadi kubwa ya wafungwa hatimaye wataachiliwa.”

UNODC imeendelea kusema kwamba “kinachotokea kwa watu wakati wa kifungo hutuathiri sisi sote kwa njia nyingi, usalama wa umma, afya yetu, fedha za jamii yetu, uwiano wa kijamii, na hatimaye heshima yetu sote ya kibinadamu. Tunapopunguza wigo wa kifungo, kuboresha hali ya magereza na kuimarisha matarajio ya kuunganishwa tena katika jamii sote tunakuwa bora zaidi. Wafungwa wana umuhimu wake.”