Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wazidi kutia giza vita dhidi ya COVID-19- Dkt. Byanyima

COVID-19 imeonyesha dhahiri kuenea kwa ubaguzi wa rangi
Unsplash/Thomas de Luze
COVID-19 imeonyesha dhahiri kuenea kwa ubaguzi wa rangi

Ubaguzi wazidi kutia giza vita dhidi ya COVID-19- Dkt. Byanyima

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umesema maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi duniani hii leo yamekuja na hisia za kipekee zaidi kwa kuzingatia jinsi ubaguzi unatishia harakati za kupambana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ambalo bado linatikisa duniani.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na UKIMWI, UNAIDS, Dkt. Winnie Byanyima katika ujumbe wake wa siku ya leo amesema virusi vya Corona vimezidisha nyufa katika jamii.

"Ingawa virusi havibagui, lakini majanga na jamii vinabagua. COVID-19 imefichua zaidi nyufa katika jamii. Imeshuhudia jamii za pembezoni ambazo tayari zilikuwa hatarini, zikiathirika zaidi kiuchumi na huduma za msingi zikizidi kuwa mashakani kwa kisingizio cha janga la Corona," amesema Dkt. Byanyima.

Amesema UNAIDS inaungana na jamii zote duniani kutak ausawa. "Tunasema kuazimia kwa HAPANA kwa aina zote za ukosefu wa usawa- iwe ni kwa sababu ya jinsia, kipato, rangi, ulemavu, jinsia unayojitambulisha nayo, kabila na dini. Aina hizo za ubaguzi na ukosefu wa usawa zinaharibu jamii yetu na kukwamisha haki na utu."

Dkt. Byanyima amesema wanachopigia upatu ni kutokomezwa kwa ubaguzi, unyanyapaa na uharamishaji wa matendo kama vile mapenzi ya jinsia moja kwa sababu ubaguzi unaua, unachochea dharura na kuongeza majanga.

"Dunia haiku kwenye mwelekeo wa kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, si kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu, uwezo au njia za kukabilia bali kwa sababu ya mifumo ya ukosefu wa usawa ambayo inakwamisha. Mathalani tafiti zinaonesha kuwa sheria za adhabu kuhusu jinsia zinaongeza maradufu uwezekano wa wanaume mashoga kupata Virusi vya Ukimwi. Kuondokana na sheria hizo ni msingi wa kutokomeza UKIMWI," amesema Mkuu huyo wa UNAIDS.

Amesema na sasa wakati wa COVID-19, ubaguzi dhidi ya wahamiaji na makundi mengine unaengua makundi kadhaa kwenye huduma za kupimwa, matibabu na usaidizi dhidi ya ugonjwa huo.

"Tunashuhudia ubaguzi ambao unatia makovu nchi zetu unafikia hata ngazi za kimataifa, Chanjo dhidi ya COVID-19 zinavyoendelea kupatikana, bado kuna ukosefu mkubwa wa uwiano. Ni nchi 10 pekee zimetoa zaidi ya asilimia 75 ya chanjo zote zilizokwishapatiwa watu duniani ilhali mataifa zaidi ya 130 hayajapata chanjo hizo. Afrika Kusini imeita virusi hivi ubaguzi wa rangi." Amesema Dkt. Byanyima.

Amesisitiza kuwa kutokomeza ukosefu wa usawa kutasongesha haki za binadamu kwa wote na kuweka dunia katika fursa nzuri ya kutokomeza COVID-19.