Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inashindwa kutekeleza ahadi ya kulinda haki za walio wachache: Guterres

Familia kutoka jamii ya Hmong ya walio wachache nchini Vietnam
© UNICEF/Truong Viet Hung
Familia kutoka jamii ya Hmong ya walio wachache nchini Vietnam

Dunia inashindwa kutekeleza ahadi ya kulinda haki za walio wachache: Guterres

Haki za binadamu

Dunia inashindwa tena vibaya sana katika ahadi yake iliyojiwekea miongo mitatu iliyopita ya kulinda haki za jamii za walio wachache amesema Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo na kuomba hatua Madhubuti zichukuliwe kukabiliana na upuuzaji huo.

Katibu Mkuu ameyasem hayo mjini New York kwenye tukio la kuadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa azimio kuhusu haki za watu wa taifa au kabilia, dini na lugha za walio wachache.

Nchi wanachama zinakutana kandoni mwa mjadala wa Baraza Kuu ili kutathimini kwa kina hatua zilizopigwa katika kutekeleza azimio hilo la kihistoria.

Kutochukua hatua na kutojali kabisa

Bwana Guterres amekuwa muwazi katika tathmini yake ya juhudi zao.

"Ukweli uliobayana ni kwamba miaka 30 baadaye dunia inafeli tena vibaya sana katika kutimiza ahadi hiyo. Hatushughulikii mapengo ,tunashughulika bila kuchukua hatua za haki na kuzembea katika ulinzi wa haki za wachache."

Wanawake ndio waathirika wakubwa

Aliripoti kwamba watu kutoka makundi ya walio wachache wamekabiliwa na kulazimishwa kuiga mambo, kuteswa, kutengwa, ubaguzi, maoni potofu, chuki, na jeuri.

Pia wamepokonywa haki zao za kisiasa na uraia, na kuona tamaduni zao zikikandamizwa, lugha zao zikikandamizwa, na mazoea yao ya kidini kubinywa.

Zaidi ya hayo, amresema zaidi ya robo tatu ya watu wasio na utaifa duniani ni wa makundi ya walio wachache, wakati janga la COVID-19 limefichua mifumo iliyokita mizizi ya kutengwa na ubaguzi unaoathiri kwa kiasi kikubwa jamii za walio wachache

"Wanawake kutoka makundi ya walio wachache mara nyingi wamekuwa wanathirika vibaya zaidi wakikabiliwa na kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia, kupoteza kazi kwa idadi kubwa, na kufaidika kidogo na msaada wowote wa  kifedha,”

Amesisitiza kuwa  wakati umefika kwa jumuiya ya kimataifa kutekeleza ahadi zake.

Wito wa kuchukua hatua

Bwana Guterres amesema "Tunahitaji uongozi wa kisiasa na hatua madhubuti. Natoa wito kwa kila nchi mwanachama kuchukua hatua madhubuti kulinda watu wa makundi ya walio wachache na utambulisho wao.”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha mwito wake wa kuchukua hatua kwa ajili ya haki za binadamu, uliotolewa Februari 2020, kama ni dira kwa serikali zote kushughulikia masuala ya muda mrefu ya ubaguzi.

Wakati huo huo, ripoti yake ya “Ajenda Yetu ya Pamoja”, iliyochapishwa Septemba mwaka jana, inataka kuwepo kwa mkataba mpya wa kijamii unaozingatia kwa kina masuala ya haki za binadamu.

Bwana Guterres amesisitiza kuwa makundi yawachache lazima washiriki kikamilifu na kwa usawa katika kila hatua na maamuzi, akiongeza kuwa ushiriki huu sio tu kwa manufaa yao.

"Sote tunafaidika. Nchi zinazolinda haki za walio wachache zina amani zaidi. Uchumi unaokuza ushiriki kamili wa walio wachache unastawi zaidi. Jamii zinazokumbatia utofauti na ushirikishwaji ni mahiri zaidi. Na ulimwengu ambamo haki za wote zinaheshimiwa ni dhabiti zaidi na wenye haki zaidi.”

Maadhimisho hayo yanapaswa kuwa kichocheo cha hatua amesema, na kuzitaka nchi kufanya kazi pamoja ili kufanya azimio hilo kuwa ukweli kwa walio wachache kila mahali.

Kuhusu Azimio

Azimio hilo la 1992 ndilo chombo pekee cha kimataifa cha Umoja wa Mataifa kinachojikita na haki za binadamu za walio wachache.

Azimio hilo linasisitiza mambo matatu ya msingi, ambayo ni kwamba haki za walio wachache ni haki za binadamu, kwamba ulinzi wa walio wachache ni muhimu kwa dhamira ya Umoja wa Mataifa, na kwamba uendelezaji wa haki hizo ni muhimu ili kuendeleza utulivu wa kisiasa na kijamii na kuzuia migogoro ndani na kati ya nchi.