Ukatili dhidi ya wanawake umeghubikwa na kimya kinachowapatia upenyo watekelezaji- Bi. Patten

25 Novemba 2019

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani, kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake inayaoshiria kuanza kwa siku 16 za harakati za kupinga ukatili kwa wanawake na wasichana.

Akihutubia washiriki, Maria Luiza Riberio Viotti ambaye ni Mkuu wa masuala ya utawala kwenye ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, “ukatili ni kitendo kibaya kwa afya ya mwili na akili, ustawi na utu kwa wasichana na wanawake, lakini pia kinadhuru familia na jamii nzima.”

Bi. Viotti amesisitiza kuwa ukatili wa kingono una madhara makubwa katika amani na usalama duniani na pia unakandamiza amani na usalama duniani.

Amekumbusha kuwa, “utamaduni wa ukatili dhidi ya wanawake una madhara makubwa katika juhudi zetu za kutokomeza umaskini na kusongesha maendeleo endelevu jumuishi. Hii ni kwa sababu unazuia wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbli za kijamii.”

Naye Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ukatili wa kingono kwenye mizozo, Pramila Patten amesema kuwa ukatili wa kingono unaohusiana na mizozo  unavuka mipaka yote na kuathiri watu wa umri na vizazi vyote na kwamba ndio vitendo ambavyo haviripotiwi ipasavyo na kwa kawaida havilaaniwi kama uhalifu wa kivita.

(Kushoto kwenda kulia mstari wa mbele) Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkuu wa UN-Women, Maria Luiza Riberio Viotti, Mkuu wa utawala ofisi ya Katibu Mkuu wa UN, Pramila Patten, Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika masuala ya ukatili wa kingono kwenye mizozo.
UN Photo/Evan Schneider
(Kushoto kwenda kulia mstari wa mbele) Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkuu wa UN-Women, Maria Luiza Riberio Viotti, Mkuu wa utawala ofisi ya Katibu Mkuu wa UN, Pramila Patten, Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika masuala ya ukatili wa kingono kwenye mizozo.

Bi. Patten amesema, “ni kimya hiki ambacho kinazuia watekelezaji huku kikiwatenga waathirika.”

Umoja wa Mataifa unasema kuwa theluthi moja ya wanawake na wasichana katika uhai wao hukumbwa na ukatili wa  kingono iwe kimwili au kiakili ambapo nusu ya wanawake waliouawa duniani kote walifanyiwa hivyo na wapenzi au familia zao.

Ukatili wa kingono dhidi ya wanawake ni sababu kuu ya vifo na majeraha kwa wale walio kwenye umri wa kuzaa kama ilivyo saratani, na pia ni sababu kuu ya afya dhoofu kuliko hata ajali za barabarani na ugonjwa wa malaria.

Tukio  hilo lilienda sambamba na tumbuizo kutoka kwa vijana wa kike na kiume wakiwa wamevalia nguo nyeusi na skafu ya rangi ya chungwa wakipazia sauti harakati za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter