Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi masikini zinalipa riba mara 4 zaidi ya Marekani na mara 8 zaidi ya nchi tajiri za Ulaya

Mwanamke akitazama huku mvua ikinyesha karibu na kituo chake cha pesa za rununu.
© IMF/Andrew Caballero-Reynolds
Mwanamke akitazama huku mvua ikinyesha karibu na kituo chake cha pesa za rununu.

Nchi masikini zinalipa riba mara 4 zaidi ya Marekani na mara 8 zaidi ya nchi tajiri za Ulaya

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti ya madeni duniani imetoka leo ambapo inaonesha viwango vya deni la umma ni vya kushangaza na vinaongezeka na viwango vya madeni yasiyo endelevu yanazidi kujilimbizika katika nchi masikini. 

Akiwa jijini New Yorka Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ujumbe wa ripoti hiyo mwaka huu ni kuwa nusu ya dunia yetu inazama katika janga la maendeleo, linalochochewa na mzozo mkubwa wa madeni. 

Amesema ripoti hiyo imebainisha watu bilioni 3.3 ambao ni karibu nusu ya wanadamu wote duniani wanaishi katika nchi ambazo hutumia zaidi hela zao kufanya malipo ya riba ya deni kuliko kuwekeza kwenye elimu au afya.

Na bado, kwa sababu madeni haya yasiyo endelevu yamejilimbikizia katika nchi maskini, hayahukumiwi kuwa hatari ya kimfumo kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa.

Riba ni kubwa sana

Madeni ni nyenzo muhimu ya kifedha ambayo inaweza kuendesha maendeleo na kuwezesha serikali kulinda na kuwekeza kwa watu wao, lakini nchi zinapolazimika kukopa kwa ajili ya kujikimu kiuchumi, deni huwa mtego ambao huzalisha deni zaidi.

Ripoti kwa mwaka 2022 inaonesha kuwa deni la umma la kimataifa lilifikia rekodi ya dola trilioni 92 za Kimarekani ambapo nchi zinazoendelea zikionekana kujitwika kiasi kisicho na uwiano.

Mapeni mengi yameonekana kushikiliwa na wakopeshaji ambao hutoza viwango vya juu vya riba kwa nchi nyingi zinazoendelea. 

“Kwa wastani, nchi za Kiafrika hulipa mara nne zaidi kwa kukopa kuliko Marekani na mara nane zaidi ya nchi tajiri zaidi za Ulaya.” Amesema Guterres 

Madeni haya ni hatari

Pamoja na ukweli kwamba madeni yasiyo endelevu yanazidi kutamalaki ulimwenguni lakini chakushangaza ni kuwa suala hili halichukuliwi kama hatari ya kimfumo kwa mfum wa kifedha wa kimataifa suala lililoonekana kumhuzunisha Katibu Mkuu Guterres 

Na bado, kwa sababu madeni haya yasiyo endelevu yamejilimbikizia katika nchi maskini, hayahukumiwi kuwa hatari ya kimfumo kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa.

“Haya ni mazingaombwe, watu bilioni 3.3 ni zaidi ya hatari ya kimfumo, ni kushindwa kimfumo. Masoko yanaweza yasiwe na shida kwas asa lakini watu wanashida. Baadhi ya nchi maskini zaidi duniani zinalazimishwa kuchagua kati ya kulipa madeni yao, au kuwahudumia watu wao lakini kwakuwa madeni haya yasiyo endelevu yamejilimbikizia katika nchi maskini, hayahukumiwi kuwa hatari ya kimfumo kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa.”

Nchi zipo katika mgogoro wa madeni

Shirika la Fedha Duniani IMF limesema nchi 36 ziko kwenye kile kinachoitwa "mgogoro wa madeni" au katika hatari kubwa ya, dhiki ya madeni. Nchi nyingine 16 wanalipa viwango vya riba visivyo endelevu kwa waliowakopesha.

Jumla ya nchi 52, karibu asilimia 40 ya nchi zinazoendelea – ziko katika matatizo makubwa ya madeni.

“Hali hii ni moja ya matokeo ya ukosefu wa usawa uliojengeka katika mfumo wetu wa kifedha wa kimataifa uliopitwa na wakati, ambao unaonesha mienendo ya nguvu ya kikoloni ya enzi ilipoundwa.” Amesema Katibu Mkuu wa UN

Ameongeza kuwa mifumo hii haijatimiza jukumu lake kama njia ya usalama kusaidia nchi zote kudhibiti msururu wa leo wa majanga yasiyotarajiwa, majanga kama athari za mabadiliko ya tabianchi na uvamizi wa Urusi kwa Ukraine.

Hatua za mabadiliko lazima zichukuliwe

Guterres amesema ripoti hii ya madeni duniani imetoa picha ya mgogoro wa madeni uliopo ulimwenguni na pia unaweka ramani ya uthabiti wa kifedha duniani, ramani ambayo ni njia ya kuelekea kwenye sera za mageuzi ya usanifu wa kifedha ulimwenguni na kichocheo ya kutimiza malengo ya SDGs. 

“Marekebisho ya kina katika mfumo wa kifedha wa kimataifa hayatafanyika mara moja. Lakini kuna hatua nyingi ambazo tunaweza kuchukua hivi sasa.” Amesema Guterres na kutoa mapendekezo 

“Mapendekezo yetu yanajumuisha utaratibu madhubuti wa kufanyia kazi deni unaoruhusu kusimamishwa kwa malipo, masharti marefu ya ukopeshaji na viwango vya chini, ikijumuisha kwa nchi zenye kipato cha kati ambazo bado hazipo imara.”

Mapendekezo mengine aliyoyataja wakati wa taarifa yake ya ripoti hii ni kuwa serikali zinaweza kukubaliana hivi sasa kuongeza ufadhili wa maendeleo na mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza msingi wa mtaji na kubadilisha mtindo wa biashara wa Benki za Maendeleo ya Kimataifa.

Amesema mapendelezo mengine yalizungumzwa katika mkutano wa kiuchumi uliofanyika nchini Ufaransa mwezi Juni2023 na mengine yatazungumzwa kwenye mkutano ujao wanchi tajiri zaidi duniani G20. 

Kusoma ripoti hiyo bofya hapa.