Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Ili kutimiza SDGs lazima tuzingatie usawa wa kijinsia

Wanawake na vijana nchini Tanzania wakikusanya taka za plastiki ambazo zitakarabatiwa na kubadilishwa kuwa vifaa vya ujenzi kama vile Matofali.
UN News/Evarist Mapesa
Wanawake na vijana nchini Tanzania wakikusanya taka za plastiki ambazo zitakarabatiwa na kubadilishwa kuwa vifaa vya ujenzi kama vile Matofali.

Guterres: Ili kutimiza SDGs lazima tuzingatie usawa wa kijinsia

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya idadi ya watu duniani ambapo mwaka huu inaangazia kuibua nguvu ya usawa wa kijinsia. Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema wakati ambapo familia ya ubinadamu ikizidi kuwa kubwa kuliko hapo awali huu ni muda wa kusimama na wanawake na wasichana na kupigania haki zao. 

Taarifa yake kutoka jijini New York Marekani imemnukuu Guterres akisema wakati huu ambapo idadi ya watu ulimwenguni ni bilioni 8 huu ni wakati wa kuimarisha azma yetu ya kufanya malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs yatimie. 

“Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku hii ya idadi ya watu duniani ni jukumu la kila mtu kuendeleza usawa wa kijinsia, kuboresha afya ya uzazi, na kuwawezesha wanawake kufanya uchaguzi wao wenyewe wa uzazi kwani ni muhimu kwao wenyewe, na muhimu katika kufikia Malengo yote ya Maendeleo Endelevu.”

Hata hivyo Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema malengo haya yanaenda mramba kwakuwa viongozi wako nyuma sana katika juhudi za kujenga dunia yenye amani na mafanikio kwa wote.

“Tukiwa nusu ya tarehe ya mwisho ya mwaka 2030 ambapo ndio tunapaswa kuyatimiza, Malengo ya Maendeleo Endelevu yamefutika kwa hatari. Lengo kama la usawa wa kijinsia litatuchukua karibu miaka 300 kulitimiza. Maendeleo kwenye masuala ya afya ya uzazi na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango yanaganda.” Amesema Guterres 

Pia amekumbusha kuwa uwekezaji kwa wanawake huleta manufaa kwa watu wote, jamii na taifa na ujumla na kinyume chake, ubaguzi wa kijinsia unamdhuru kila mtu iwe ni wanawake, wasichana, wanaume na wavulana. 

Udhalimu dhidi ya wanawake

Ingawa idadi yao ulimwenguni ni sawa na asilimia 49.7, lakini wanawake na wasichana mara nyingi hupuuzwa katika mijadala kuhusu idadi ya watu, huku haki zao zikikiukwa katika sera za idadi ya watu.

Udhalimu huu ulioenea huwafanya wanawake na wasichana wasiende shule, kuukosa kazi na nafasi za uongozi, hali hii inapunguza uwakilishi na uwezo wao wa kufanya maamuzi kuhusu afya zao na uzazi wa mpango.

Pia huongeza uwezekano wa kukabiliwa na unyanyasaji, mila zenye madhara na vifo vinavyoweza kuzuilika vya uzazi, huku mwanamke akifariki kila baada ya dakika mbili kutokana na ujauzito au kujifungua.

Siku ya idadi ya watu ni ukumbusho kwetu

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA Dk. Natalia Kanem amesema siku ya Idadi ya Watu Duniani ni ukumbusho kwamba mustakabali mzuri zaidi, wa amani na endelevu unaweza kufikiwa “ikiwa tutatumia nguvu za kila mwanadamu kwenye sayari.”

Ujumbe wake kwa Siku hiyo ulionesha kwamba zaidi ya asilimia 40 ya wanawake duniani kote hawawezi kutumia haki yao ya kufanya maamuzi ya msingi kama vile kupata watoto au la.

Usawa kijinsia unanufaisha wote

“Kuwawezesha wanawake na wasichana, ikiwa ni pamoja na kupitia elimu na upatikanaji wa uzazi wa mpango wa kisasa, kunasaidia kuwasaidia katika matarajio yao na kupanga njia ya maisha yao," alisema.

Dk. Kanem amesisitiza kuwa kuendeleza usawa wa kijinsia ni suluhisho mtambuka kwa matatizo mengi ya kijamii.

Alisema kwa jamii zinazozeeka zinazohofia tija ya kazi, kufikia usawa wa kijinsia mahali pa kazi inawakilisha njia bora zaidi ya kuboresha pato na ukuaji wa uchumi.

“Wakati huo huo, katika nchi zinazokabiliwa na ongezeko la kasi la idadi ya watu, uwezeshaji wa wanawake kupitia elimu na upangaji uzazi unaweza kuleta manufaa makubwa kwa njia ya mtaji wa binadamu na ukuaji wa uchumi shirikishi.” aliongeza.

Dk. Kanem alisema suluhisho liko wazi, kwani “kuharakisha maendeleo ya usawa wa kijinsia - kupitia upatikanaji wa afya na haki za ujinsia na uzazi, elimu bora, sera zinazofaa za kazi, na kanuni za usawa mahali pa kazi na nyumbani kutasababisha familia zenye afya, uchumi imara, na jamii zinazostahimili uthabiti.”

UNFPA inafanya nini kuwasaidia?

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA linatekeleza miradi kadhaa katika nchi mbalimbali duniani lengo likiwa ni kuwaandaa wanaume na wasichana kuwa watetezi wa haki.

Dk. Kanem amesema, “Tunapofungua uwezo kamili wa wanawake na wasichana, kuhimiza na kuzikuza haja za mioyo yao ili waweze kufikia malengo yao, kazi zao na familia zao tunachochea nusu ya uongozi, mawazo, uvumbuzi, na ubunifu kwa jamii bora.”