Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tutokomeze aina zote za ukatili kwa wanawake na wasichana:UN

Siku ya kimataifa ya kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake
UN Women
Siku ya kimataifa ya kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake

Lazima tutokomeze aina zote za ukatili kwa wanawake na wasichana:UN

Wanawake

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana, Umoja wa Mataifa umesema umedhamiria kukomesha mifumo yote ya ukatili kwa kundi hilo kwani ni wajibu na haki kufanya hivyo. 

Kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ukatili huu ni miongoni mwa ukatili mbaya zaidi duniani, unaoendelea na ukiukwaji mkubwa kabisa wa haki za binadamu uliosambaa, ukiathiri mtu mmoja miongoni mwa kila wanawake watatu duniani.Ameongeza kuwa hii inamaanisha kwamba mtu mmoja karibu nawe, jamaa wa familia, mfanyakazi mwenzako, rafiki yako au hata wewe mwenyewe unakugusa.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana haujaanza leo chimbuko lake ni karne za mfumo dume, “hebu tusisahau kwamba pengo la usawa wa kijinsia ambalo limechochea utamaduni wa ubakaji ni suala la kutokuwepo na uwiano wa mamlaka. Unyanyapaa, dhana potofu, kutoripotiwa vya kutosha na utekelezwaji duni wa sheria kunachochea ukwepaji wa sheria na ubakaji bado unatumika kama silaha mbaya ya vita.”

Hivyo amesema yote haya sasa ni lazima yabadilike na kutoa wito kwa serikali zote, sekta binafsi, asasi za kiraia na watu kila mahali kuchukua msimamo thabiti dhidi ya dhuluma za kijinsia na ujinga. Amemshihi kila mmoj kuonyesha mshikamano mkubwa na waathirika, watetezi na wapigania haki za wanawake na kwamba“Lazima tuchagize haki za wanawake na fursa sawa. Pamoja, tunaweza na lazima tumalize ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia wa kila aina.”

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Phumzile Mlambo- Ngcuka akiunga mkono hayo ametoa wito wa kutokomeza moja ya ukatili mkubwa kabisa ambao ni ubakaji, madhila yake na gharama zake zisizovumilika kwa wanawake na jamii, Endapo ningekua na tamanio langu moja litakalotimizwa linaweza kuwa ni kutokomeza kabisa ubakaji na mifumo yote ya ukatili dhidi ya wanawake. Ubakaji sio tukio tu la kipekee lina athari kubwa za kubadili maisha, mimba au magonjwa ya zinaa, kiwewe kikubwa na aibu. Wakati wote wa amani au wa vita unakuwa sababu ya maamuzi ya wanawake kuondoka katika jamii zao kwa kuhofia kushambuliwa.”

Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana huadhimishwa kila mwaka Novemba 25, siku ambayo pia huanza siku 16 za harakati za uchagizaji na uelimishaji kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.