Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Ukraine na Urusi wana jukumu muhimu kuhakikisha upatikanaji wa chakula duniani

Timu za ukaguzi wa pamoja zikifanya kazi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.
© UNODC/Duncan Moore
Timu za ukaguzi wa pamoja zikifanya kazi chini ya Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi.

Guterres: Ukraine na Urusi wana jukumu muhimu kuhakikisha upatikanaji wa chakula duniani

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo amekumbusha jukumu muhimu na la lazima za kuuza chakula na mbolea zinazotoka katika nchi za Ukraine na Urusi mtawalia ingawa nchi hizo kwa sasa zipo katika mzozo. 

Taarifa kwa vyombo vya habari ilitotolewa na Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu Farhan Haq jijini New York Marekani imesema Katibu Mkuu ameeeleza nchi hizo mbili zina mchango mkubwa katika kuhakikisha kuna uhakika wa upatikanaji wa chakula duniani. 

Guterres amesisitiza umuhimu wa utekelezaji kamili na endelevu wa makubaliano yaliyotiwa saini huko Istanbul mwezi Julai 2022, kusaidia kuhakikisha bidhaa hizo zinaweza kufikia masoko ya kimataifa kwa urahisi, kwa ufanisi na kwa kiwango.

“Makubaliano haya ni onyesho la nadra sana la kile ambacho ulimwengu unaweza kufanya inapoweka mawazo yake kwenye changamoto kuu tuliyonayo kwa sasa. Kwa pamoja, mikataba hiyo inachangia kupungua kwa bei ya chakula duniani kote, ambayo sasa ni zaidi ya asilimia 23 chini ya rekodi ya juu iliyofikiwa Machi 2023.” Amesem Guterres

Katibu Mkuu Guterres ameeleza kuwa yeye pamoja na timu yake wanaendelea kujitolea kikamilifu kuendeleza maendeleo ambayo tayari yamepatikana na wanawasiliana mara kwa mara na wadau mbalimbali katika suala hili. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa wote wanaohusika na masuala mbalimbali kuhakikisha kuwa kwenye kila kitu wanachofanya wanatanguliza dunia ina uhakika wa upatikanaji wa chakula.