Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjini Port Sudan, UNFPA inasaidia kuhakikisha uzazi salama kwa wanawake na wasichana wanaokimbia ghasia Khartoum

Wakunga wawili wakifanya kazi katika kliniki inayoungwa mkono na UNFPA nchini Sudan. (faili)
© UNFPA Sudan
Wakunga wawili wakifanya kazi katika kliniki inayoungwa mkono na UNFPA nchini Sudan. (faili)

Mjini Port Sudan, UNFPA inasaidia kuhakikisha uzazi salama kwa wanawake na wasichana wanaokimbia ghasia Khartoum

Wanawake

Wanawake  na wasichana wanaokimbia machafuko yanayoendelea mjini Kharthoum nchini Sudan wanakabiliwa na changamoto lukuki hususan kwa wajawazito wanaohitaji msaada wa kujifungua, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA ambalo sasa limechukua jukumu la kuhakikisha uzazi salama kwa wanawake hao.

Miongoni mwa wanawake hao ni Omnia hili si jina lake halisi amepewa ili kulinda usalama wake, akiwa na ujauzito wa miezi tisa,  alilazimika kuacha nyumba yake na kila kitu alichojua ili kuepuka vita kali iliyoukumba mji mkuu wa Sudan, Khartoum kuokoa maisha yake.

Kwa uchumngu mkubwa anasema "Nimepoteza kila kitu katika vita hii. Lakini sikutaka kumpoteza mtoto wangu ambaye bado hajazaliwa.”

Ingawa kusafiri katika hali yake ilikuwa hatari, alihisi hakuwa na chaguo, ukosefu wa usalama, risasi zinazorindima, uporaji na uharibifu wa vituo vya afya ulimaanisha kuwa hakuweza kumuona daktari kwa wiki kadhaa, ilikuwa safari ngumu ya siku tano, hatimaye mapema Juni alifanikiwa kufika Port Sudan, kwenye ufuo wa jimbo la bahari ya Sham.

Omnia alikuwa akilia njia nzima kutoka Khartoum na aliogopa kwamba angepata uchungu na kujifungulia njiani kuelekea Port Sudan.

Kwa mujibu wa UNFPA Omnia ni kisa kimoja tu lakini maelfu ya wanawake na wasichana wanapitia changamoto hiyo hivi sasa Sudan. 

Alikuwa na bahati kwani aliwasili katika hospitali ya mafunzo ya Port Sudan ambako alianza kuumwa uchungu na kusaidiwa kujifungua salama mtoto wa kike kwa njia ya upasuaji. 

Hata hivyo UNFPA inasema “hiyo ni hospital pekee ya serikali inayotoa huduma za uzazi kwa watu milioni 1.6  na sasa shirika hilo la idadi ya watu na wadau wa bahari ya Sham wanaisaidia hospitali hio kwa vifaa, dawa na mafunzo kwa wahudumu ili kuhakikisha wakina mama wajawazito kama Omnia waliotawanywa na vita na kuwasili Port Sudan kutoka nchi nzima wanajifungua salama.”

Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Randa Osman anasema “Timu yetu imejitolea kikamilifu kusaidia wanawake na wasichana wanaowasili kutoka Khartoum, lakini tunahitaji vifaa zaidi vya dharura, ikiwa ni pamoja na mafuta na vifaa vya kuokoa maisha na dawa. “

Kwa mujibu wa UNFPA takriban vituo 46 vya afya nchini Sudan vimeshambuliwa, na karibu theluthi mbili havifanyi kazi tena.

Mpango wa hivi karibuni wa msaada wa kibinadamu Sudan unalenga kuwasaidia waty milioni 24.7 ambapo milioni 11 kati yao wanahitaji msaada wa dharura wa huduma za afya na wanawake na wasicha milioni 2.6 miongoni mwao wako katika umri wa kuzaa.