Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNITAMS yakaribisha usitishaji mapigano Sudan wakati wa Eid Al-Haj

Mama na binti zake wanne wanawasili Chad kutoka Sudan.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Mama na binti zake wanne wanawasili Chad kutoka Sudan.

UNITAMS yakaribisha usitishaji mapigano Sudan wakati wa Eid Al-Haj

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi wa mpito nchini Sudan UNITAMS, leo umekaribisha usitishaji vita wa upande mmoja wa jeshi la Sudan SAF na vikosi vya msaada wa haraka RSF, katika sikukuu za Eid na kusisitiza haja ya vikosi vyote viwili kudumisha muafaka huo.

Wakati huo huo, RSF na wanamgambo washirika wake wanaendelea kuwajibika kwa unyanyasaji dhidi ya raia, ubakaji na uporaji katika maeneo wanayodhibiti, ikiwa ni pamoja na Khartoum, na ghasia zenye mlengo wa kikabila dhidi ya raia huko Darfur imesema taarifa ya ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa uliotolewa leo mjini Khartoum.

 UNITAMS imesema “SAF inasalia kuwajibika kwa mashambulizi katika maeneo yenye wakazi wengi wa kiraia, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya angani katika maeneo ya makazi ya watu mjini Khartoum. Chini ya sheria za kimataifa, pande zinazopigana zinawajibika kwa ulinzi wa raia katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao.”

Ujumbe huo umesisitiza kwamba “Eid al-Haj iwe ukumbusho kwamba vurugu lazima zikome. Raia wanapaswa kuishi kwa amani na sio kwa fujo za pande zinazopigana. Pande zote zinapaswa kukumbushwa kwamba ulimwengu unatazama na uwajibikaji kwa uhalifu uliofanywa wakati wa vita utafuatiliwa.”