Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taliban wanaweza kuwajibika kwa ubaguzi wa kijinsia Afghanistan: UN

© UN Human Rights/Petre Oprea
Volker Türk (kulia), Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 53 cha
© UN Human Rights/Petre Oprea

Taliban wanaweza kuwajibika kwa ubaguzi wa kijinsia Afghanistan: UN

Haki za binadamu

Masaibu ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan leo yamepewa uzito katika Baraza la Haki za binadamu ambapo wataalam huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wameonya kuhusu ubaguzi wa kijinsia na unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea katika taifa hilo.

Volker Türk, kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu, ameelezea wasiwasi kama huo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la haki za binadamu cha majira ya joto, na kuongeza kuwa mamlaka ya Taliban "imevunja kanuni za msingi zaidi za haki za binadamu, hasa kwa wanawake na wasichana".

Katika ripoti ya pamoja iliyowasilishwa kwa Baraza na mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afghanistan na kikosi kazi kuhusu ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana, wataalam hao, Richard Bennett na Dorothy Estrada-Tanck, wamesema “masaibu ya wanawake na wasichana hao ni miongoni mwa mabaya zaidi duniani.”

Ripoti yao inatoa wito kwa mamlaka ya Taliban kuheshimu na kurejesha haki za binadamu za wanawake na wasichana. 

Pia inahimiza jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuzingatia zaidi hali ya ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan.

© UNOCHA/Charlotte Cans
Mfanyikazi wa OCHA akizungumza na wanawake waliokimbia makazi yao katika jimbo la mashariki la Nangahar nchini Afghanistan.
© UNOCHA/Charlotte Cans

Upendeleo wa kiitikadi

Bwana Bennett amesema "Pia tumelielezea baraza wasiwasi wetu mkubwa kwamba kunyimwa kwa haki za msingi za wanawake na wasichana na utekelezaji mkali wa hatua za kizuizi unaofanywa na mamlaka ya Taliban kunaweza kujumuisha na kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu wa unyanyasaji wa kijinsia," 

Wameongeza kuwa "Ubaguzi mkubwa, wa kimfumo na wa kitaasisi dhidi ya wanawake na wasichana ndio kiini cha itikadi na sheria ya Taliban, ambayo pia inazua wasiwasi kwamba wanaweza kuwajibika kwa ubaguzi wa kijinsia."

Akirejelea wasiwasi huo, naibu kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu, Nada Al-Nashif amesisitiza kwamba “licha ya madai kinyume ya mara kwa mara ya utawala huo, katika muda wa miezi 22 iliyopita, kila nyanja ya maisha ya wanawake na wasichana imewekewa vikwazo. Wanabaguliwa kwa kila namna.”

Bwana Bennett, ambaye alitembelea Kabul na Mazar-e-Sharif nchini Afghanistan kutimiza jukumu lake la mtaalamu maalum, amethibitisha kwamba hakuweza kuripoti uboreshaji wa hali ya haki za binadamu "hakika si kwa wanawake na wasichana ambao hali yao imezidi kuwa mbaya zaidi, wala kwa wengine katika idadi ya watu waliotengwa, wanaohusishwa na jamhuri ya zamani ya Kiislamu, au wanaopinga au hata kutokubaliana na itikadi ya Taliban”.

Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.
IOM/Robert Kovacs
Wasichana wa Afghanistan wanawasili nchini Rwanda kuendelea na masomo.

Kuhisi kuzikwa ukiwa hai

Akitoa tathimini ya kina juu ya mawazo ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan, Shaharzad Akbar, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali au NGO ya Afghanistan Rawadari, ameliambia Baraza kwamba wanazungumza juu ya "kuzikwa wakiwa hai, wanapumua lakini hawana uwezo wa kufanya mengi zaidi bila kukabiliwa na vikwazo na adhabu,  maisha yao yamekwama huku maisha ya wanaume waliowazunguka, watoto wao wa kiume, ndugu zao, waume zao yakisonga mbele.”

Bi Akbar pia ameangazia pengo kati ya utawala wa Taliban na nchi nyingine jirani za Kiislamu ambapo wanawake wanaruhusiwa kutafuta elimu, kutekeleza ndoto zao, kusafiri anga za juu, na kushiriki katika siasa.

Lakini sio Afghanistan, ambapo "Taliban wameigeuza Afghanistan kuwa kaburi kubwa la matarajio ya wanawake na wasichana wa Afghanistan, la kuzima ndoto na uwezo wao".