Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani shambulio la Kabul na kukumbusha wajibu wa kulinda raia

Baada ya mlipuko katikati ya mji mkuu wa Afghanistan Kabul
UNAMA/Jawad Jalali (file)
Baada ya mlipuko katikati ya mji mkuu wa Afghanistan Kabul

UN yalaani shambulio la Kabul na kukumbusha wajibu wa kulinda raia

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameelezea kugadhabishwa na kusikitishwa na mashambulizi yaliyotekelezwa na kundi la waasi la Taliban kwenye eneo la raia wengi lililopo mji mkuu wa Afghanistan, Kabul  tarehe mosi mwezi huu wa Julai.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu iliyotolewa jijini New York, Marekani,  utafiti wa awali unaonesha kwamba shambulio hilo limesababisha majeruhi zaidi ya 100 wakiwemo wanawake na watoto. 

Aidha vilipuzi hivyo vimesababisha uharibifu wa shule na miundombinu mingine katika vitongoji vya eneo la tukio.

Taarifa ya Katibu Mkuu imemnukuu akikumbusha kwamba sheria ya kimataifa inazuia mashambulizi ya kulenga raia na ametolea wito pande husika katika mzozo wa Afghanistan kuzingatia wajibu wao katika kulinda raia.

Bwana Guterres ameelezea kusikitishwa na tukio hilo na kutoa pole zake kwa familia na waathirika na serikali na watu wa Afghanistan. Aidha amewatakia afueni ya haraka majeruhi.

Wakati huo huo Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto kwenye mizozo, Virginia Gamba ameelezea kusikitishwa na shambulizi hilo ambalo watoto wa kike na kiume wameuawa au kujeruhiwa kufuatia kupuuzwa kwa sheria za vita kwa mfano ulinzi wa watoto na maeneo salama wakati wa mashambulizi.

Bi. Gamba ameongeza kwamba watoto wana haki ya kulindwa wakati wote hususan wakiwa shuleni au nyumbani.

Ameelezea kusikitishwa kwake na kuendelea kwa ukatili unaotekelezwa an kundi la Taliban na wengine katika mzozo nchini Afghanistana na kutoa wito kwa hatua muafaka kuchukuliwa kwa ajili ya ulinzi na uslama wa watoto ambao huwa hatarini zaidi wakati wa vita.

 

TAGS: Kabul. Taliban, Afghanistan, Antonio Guterres, Virginia Gamba