Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la kudumu la watu wa asili ya Afrika limeng’oa nanga UN

Mmoja wa wanachama wa kampuni ya ngoma ya Batoto Yetu akitumbuiza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Pili cha Jukwaa la Kudumu la Watu Wenye Asili ya Afrika, New York, Marekani.
UN Photo/Loey Felipe
Mmoja wa wanachama wa kampuni ya ngoma ya Batoto Yetu akitumbuiza wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Pili cha Jukwaa la Kudumu la Watu Wenye Asili ya Afrika, New York, Marekani.

Jukwaa la kudumu la watu wa asili ya Afrika limeng’oa nanga UN

Haki za binadamu

Jukwaa la pili la kudumu kuhusu watu wenye asili ya Afrika limeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani na litaendelea hadi tarehe 2 Juni.

 

Mada kuu zinazojadiliwa katika siku nne za jukwaa hili “zitajikita katika haki za binadamu zikimulika masuala kama haki ya upatanisho wa kimataifa, Pan-Africanism kwa ajili ya utu, haki na amani, uhamiaji wa kimataifa, kutambua na kushughulikia ubaguzi wa kimfumo na kimuundo kwa kuzingatia takwimu na Ushahidi, na afya, ustawi, na kiwewe kilichodumu kati ya vizazi.”

Lengo kuu la nada zinazojaliwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni kuchangia kwenye mchakato wa kutanabaisha uchagizaji wa azimio la Umoja wa Mataifa la kuchagiza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu za watu wenye asili ya Afrika.

Haki kwa watu wenye asili ya Afrika

Akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu wa jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Kuanzishwa kwa jukwaa hili na Baraza Kuu kulionyesha dhamira ya jumuiya ya kimataifa ya kuongeza kasi katika njia ya kuelekea usawa kamili na haki kwa watu wa asili ya Kiafrika kila mahali.”

Ameongeza kuwa “Jumuiya ya asili ya Kiafrika ugahibuni imeongeza  tija na kutajirisha jamii katika kila kona ya dunia na kuchangia pakubwa katika kila nyanja ya jitihada za binadamu. Na hicho ndicho tunasherehekea hapa leo.”

Hata hivyo amesema pamoja na mchango wao mkubwa “Bado, tunafahamu kwa uchungu kwamba watu wenye asili ya Kiafrika wanaendelea kukabiliana na ubaguzi wa rangi uliokita mizizi na ubaguzi wa kimfumo. Karne nyingi za kivuli cha utumwa na unyonyaji wa kikoloni bado kinaharibu maisha yetu ya sasa.”

Wakati wa kurekebisha makosa ni sasa

Bwaba Guterres amesisitiza kwamba “Wakati kutambua na kurekebisha makosa ya muda mrefu umepita. Ni lazima tuchukue hatua haraka zaidi sasa ili kuziondoa jamii zetu katika janga la ubaguzi wa rangi, na kuhakikisha ushirikishwaji kamili wa kisiasa, kiuchumi na kijamii wa watu wa asili ya Kiafrika kama raia sawa na wengine, bila ubaguzi.”

Ameongezea kuwa na hilo ndilo lengo la Mpango Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kushughulikia Ubaguzi wa Rangi na Kukuza Utu kwa Wote.

Amewashukuru washiriki wa kujwaa hilo kwa kujumuika pamoja ili kubadilishana mawazo na mikakati ya kusaidia ulimwengu kusonga mbele na kuachana na ubaguzi.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusistiza kuwa “Kwa pamoja, hebu hatimaye tutambue mustakabali wa utu, fursa, na haki kwa wote.”