Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yataka hatua zaidi kumaliza ukoloni kwenye maeneo 17 duniani

Tomasi Tafia, Meneja Mkuu wa Nishati, akifafanua jinsi umeme unaotokana na jua unavyobadilishwa kuwa umeme katika mradi wa majaribio wa nishati mbadala, unaoungwa mkono na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Ariane Rummery
Tomasi Tafia, Meneja Mkuu wa Nishati, akifafanua jinsi umeme unaotokana na jua unavyobadilishwa kuwa umeme katika mradi wa majaribio wa nishati mbadala, unaoungwa mkono na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa.

UN yataka hatua zaidi kumaliza ukoloni kwenye maeneo 17 duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mawazo mapya na njia mpya za kuondokana na zama za ukoloni ni muhimu zaidi hivi sasa ili hatimaye kuweza kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs katika maeneo 17 ambayo bado yanatawaliwa. 

Ni kauli yake hiyo aliyotoa kwa njia ya video kwenye semina ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuondokana na ukoloni, semina iliyofanyika mjini Bali, Indonesia. 

Semina hiyo imefanyika kwenda sambamba na wiki ya kuonesha mshikamano na watu na maeneo ambayo bado yanataliwa duniani inayomulikwa tarehe 25 hadi 31 mwezi Mei kila mwaka. 

“Lengo letu la pamoja ni kupatia kipaumbele kikubwa ajenda ya kuondokana na ukoloni na kuchochea kasi ya uchukuaji hatua,” amesema Guterres kwa wajumbe wa semina ya kikanda ya Kamati Maalum ya kuondokana na Ukoloni au C-24. 

Kamati hiyo ilianzishwa na Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa mwaka 1961, ikiwa na jukumu la kuchunguza maombi ya Azimio la kupatia uhuru nchi zinazotawaliwa pamoaj na watu wake. 

Tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa mwaka 1945, zaidi ya makoloni 80 ya zamani yakiwa na jumla ya watu milioni 750 aymeshapata uhuru. Mchakato wa sasa unalenga maeneo 17 yasiyojitawala, yakiwa na watu tarkibani milioni 2. 

Kuangazia SDGs 

Akimulika maudhui ya semina hiyo, Kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kwenye maeneo hayo, Katibu Mkuu amesema ikiwa imesalia nusu ya kufikia ukomo wa malengo hayo, “tunaacha nyumba zaidi ya nusu ya wakazi wa dunia.” 

Maendeleo yamekwama, na katika maeneo mengine, maendeleo yamerudi nyumba,” ameonya Katibu Mkuu. 

Amesema kuwa SDGs ni njia ya amani na ustawi kwa wote kwenye sayari yenye afya; hakuna nchi inayoweza kukubali kuona malengo hayo yanashindikana. 

Changamoto dhahiri 

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema kwa maeneo mengi ambayo bado yanatawaliwa, na ambayo ni nchi za visiwa vidogo vilivyo mstari wa mbele vikikumbana na dharura ya madhara ya tabianchi, hali ni dhahiri kabisa. 

“Kama jamii ya kimataifa, lazima tuhakikishe maeneo hayo yana rasilimali na msaada unaohitajika kusongesha SDGs, kujenga mnepo na kuwekeza kwa ajili ya siku za usoni,” amewaeleza wajumbe wa semina hiyo. 

Mchakato wa kutokomeza ukoloni lazima uongozwe na matamanio na mahitaji ya maeneo hayo kwa kuzingatia kila eneo lilivyo, amesema Katibu Mkuu akitoa shukrani zake kwa Kamati hiyo kwa kujizatiti kwake bila kuchoka kukamilisha utokomezaji wa ukoloni duniani. 

Watoto wanacheza kwenye jeti kwenye Kisiwa cha Fale katika visiwa vya Bahari ya Pasifiki vya Tokelau.
© UNICEF/Vlad Sokhin
Watoto wanacheza kwenye jeti kwenye Kisiwa cha Fale katika visiwa vya Bahari ya Pasifiki vya Tokelau.

Kubadili mwelekeo 

“Nawategemea ninyi kuchochea mawazo mapya na kufungua njia mpya za ushirikiano thabiti kati ya maeneo, watawala na wadau wengine kwa mujibu wa maazimio husika,” amesema Guterres. 

Amesisitiza kuwa kwa pamoja wanaweza kubadili mwelekeo na kuchagiza njia mpya ya kufanikisha SDGs kwenye maeneo husika na kwingineko. 

Kufahamu zaidi kuhusu jinsi UN inasaidia kuondokana na ukoloni bofya hapa