Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho jipya la mapigano kwa muda mfupi Sudan kuanza kutekelezwa leo- Perthes

Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kupokea vifaa muhimu vya msaada kakati wa usambazaji huko Koufroun, kijiji cha Chad karibu na mpaka wa Sudan.
© UNICEF/Donaig Le Du
Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kupokea vifaa muhimu vya msaada kakati wa usambazaji huko Koufroun, kijiji cha Chad karibu na mpaka wa Sudan.

Sitisho jipya la mapigano kwa muda mfupi Sudan kuanza kutekelezwa leo- Perthes

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuwa makubaliano ya sitisho la muda mfupi wa mapigano kati ya pande kinzani kwenye mapigano yanayoendelea nchini Sudan yanaanza kutekelezwa hii leo. 

Akihutubia Baraza hilo leo jijini New York, Marekani, Bwana Perthes ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia kipindi cha mpito SUDAN, UNITAMS amesema makubaliano hayo ya muda mfupi yalitiwa saini tarehe 20 mwezi huu wa Mei huko Jeddah, Saudi Arabia. 

“Shukrani kwa usuluhishi wa Saudia na Marekani, wawakilishi wa jeshi la serikali ya Sudan, SAF na wale wa wanamgambo wa Rapid Support Forces, RSF, walitia saini Azimio la ahadi ya utekelezaji tarehe 11 mwezi Mei, na makubaliano ya sitisho la muda mfupi la mapigano tarehe 20 Mei. Makubaliano hayo ya sitisho la mapigano kwa muda mfupi yanapaswa kuanza kutekelezwa usiku wa leo,” amesema Bwana Perthes. 

Sitisho la mapigano la muda mfupi ni kwa siku 7 

Amesema makubaliano hayo yatazingatiwa kwa siku saba na yanaweza kuwekwa saini na kutumika tena na kwamba itapaswa kuruhusu raia kutembea na pia misaada ya kibinadamu ifikie raia hao. 

“Hii ni hatua ambayo tunaikaribisha kwa sababu mapigano na  hama  hama ya wanajeshi vimeendelea hata leo hii, licha ya ahadi ya pande zote mbili ya kutoendelea na mapigano kabla ya kuanza kutekelezwa kwa sitisho la mapigano,” amefafanua Mkuu huyo wa UNITAMS. 

Bwana Perthes amesema ni matumaini yake kuwa pande mbili husika zitaweka mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa sitisho hilo la mapigano la muda mfupi na kwamba UNITAMS imesimama kidete kusaidia mfumo kama huo. 

Amesisitiza kuwa ni matumaini yake sitisho hili la muda mfupi la mapigano linaweza hatimaye kufanikisha kupatikana kwa sitisho la kudumu la mapigano. 

Vipaumbele vya UNITAMS kwa sasa 

UNITAMS inasalia na vipaumbele vyake vinne ambavyo ni mosi; kufanikisha makubaliano thabiti ya sitisho la mapigano na mfumo wa ufuatiliaji; pili kuzuia ongezeko la mapigano au mzozo huo kuenea kwa misingi ya kikabila; tatu kulinda raia na kutoa misaada ya kibinadamu na nne; kujiandaa, pindi wakati utakuwa muafaka mchakato mpya wa kisiasa wenye ushiriki wa pande mbali mbali za kiraia, wanasiasa pamoja na wanawake. 

Mapigano kati ya SAF na RSF yalianza kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum na hadi tarehe 17 mwezi huu wa Mei jumla ya watu 676 wameuawa, wengine 5,576 wamejeruhiwa, watu 200,000 wamekimbilia nchi jirani huku 736,200 ni wakimbizi wa ndani.