Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono vyashamiri kwenye kambi za wakimbizi wa ndani DRC 

Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao.
© UNHCR/Blaise Sanyila
Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono vyashamiri kwenye kambi za wakimbizi wa ndani DRC 

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu  nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Bruno Lemarquis amezungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo na kusema vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono dhidi ya wanawake na wasichana kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani nchini DRC vimeongezeka kwa asilimia 37 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana, huku akitaka hatua za haraka zichukuliwe ili kurekebisha kinachoendelea.

Katika mkutano wake huo uliomulika hali ya kibinadamu nchini DRC, Bwana Lemarquis ambaye pia ni Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC amesema mwaka jana pekee kwenye makazi ya wakimbizi katika jimbo la Kivu Kaskazini, kulikuwa na matukio zaidi ya 38,000 ya ukatili wa kingono na kwamba katika miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu pekee, kumekuweko na ongezeko kwa asilimia 37. 

Amesema “wanawake na watoto walio hatarini zaidi ambao wanasaka hifadhi kwenye makazi hayo, wanajikuta wakikabiliwa na ukatili na machungu zaidi na hili halivumiliki.” 

Hivyo amesema hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa na serikali pamoja na wadau ili kudhibiti hali hiyo. 

Lemarquis amesema ongezeko la wakimbizi wa ndani kwenye makazi linatokana pia na ombwe la ulinzi kwenye maeneo ya kaskazini mwa jimbo la Kivu Kaskazini, Ituri na Kivu Kusini kutokana na vikosi vya usalama kuhamishwa ili kwenda kukabiliana na waasi wa M23. 

Amesema baadhi ya makundi yaliyojihami kama vile ADF, Zaire na CODECO yametumia fursa hiyo kushamirisha mashambulizi yao dhidi ya raia hususan Ituri. 

Naibu Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu nchini DRC amegusia pia jimbo la Mai-Ndombe lililoko magharibi mwa DRC, ambako amesema ghasia zilizoibuka mwezi Juni mwaka jana zimeendelea na zinasambaa kwenye maeneo ya jirani na kwamba kwa kuwa DRC inaelekea kwenye uchaguzi ni vema kuchukua hatua kudhibiti ili ghasia hizo zisijekuwa chanzo cha janga lingine la kibinadamu nchini humo.