Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua mtandao wa kimataifa wa kubaini na kuzuia tishio la magonjwa ya kuambukiza

Daktari akichambua sampuli katika maabara ya hospitali ya mafunzo nchini Nigeria
© WHO/Etinosa Yvonne
Daktari akichambua sampuli katika maabara ya hospitali ya mafunzo nchini Nigeria

WHO yazindua mtandao wa kimataifa wa kubaini na kuzuia tishio la magonjwa ya kuambukiza

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO hii leo kwa ushirikiano na wadau wamezindua mtandao wa kimataifa wa kusaidia kulinda watu dhidi ya tishio la magonjwa ya kuambukiza kupitia mfumo wa uchambuzi wa kanuni za kijenetiki za virusi,  bakteria na vijiumbe maradhi vingine vinavyosababisha magonjwa.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema Mtandao huo wa kimataifa wa usimamizi na ufuatiliaji wa vijidudu, IPSN utakuwa ndio jukwaa la kuunganisha nchi na kanda, kuimarisha mifumo ya kukusanya na kuchambua sampuli, na kutumia data hizo ili kuchochea uamuzi katika masuala ya afya ya umma na zaidi ya yote kubadilishana taarifa hizo kwa mapana zaidi.

Mfumo huo wa uchambuzi wa kanuni za kijenetiki za virusi na bakteria pamoja na vijiumbe maradhi vingine visababishavyo magonjwa, utawezesha kuelewa ni kiwango cha vijidudu hivyo kusababisha maambukizi, hatari za maambukizi yake na jinsi vinasambaa.

“Kuweko kwa taarifa hizo kutasaidia wanasayansi na maafisa katika sekta ya afya ya umma kubaini na kufuatilia magonjwa, kuzuia na kuchukua hatua kudhibiti milipuko kama sehemu ya mifumo ya ufuatiliaji magonjwa na vile vile kutengeneza tiba na chanjo,” imesema taarifa hiyo.

Akizungumzia mtandao huu wa IPSN, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema lengo la mtandao huu mpya ni la juu mno lakini linaweza pia kuwa na dhima muhimu katika usalama kwenye afya: kupatia kila nchi fursa ya kupata uchambuzi wa vijidudu kijenetiki kama sehemu ya mfumo wao wa afya, kama ilivyobainika wakati wa janga la coronavirus">COVID-19, dunia iko thabiti zaidi pindi tunaposimama pamoja kukabili vitisho vya afya.”

WHO ndio sekretarieti ya IPSN ambayo ina wataalamu kutoka pande mbali mbali wakiwemo wataalamu wa uchambuzi wa data za kijenetiki, serikalini, wakfu za utoaji misaada, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia, wanazuoni na sekta binafsi.