Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msizike marehemu wa majanga kwenye makaburi ya halaiki: WHO

Timu za Red Crescent zinasaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko kaskazini mashariki mwa Libya.
© Libyan Red Crescent
Timu za Red Crescent zinasaidia jamii zilizoathiriwa na mafuriko kaskazini mashariki mwa Libya.

Msizike marehemu wa majanga kwenye makaburi ya halaiki: WHO

Haki za binadamu

Kunapotokea majanga au vita na kusababisha watu wengi kupoteza maisha kunakuwa na hofu kuhusu miili ya marehemu kuwa inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa hivyo baadhi ya jamii kwakutokuwa na taarifa sahihi hujikuta wakizika miili hiyo katika makaburi ya halaiki ili kuepuka mlipuko wa magonjwa lakini shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO linasema hiyo si sahihi. 

Kuzika marehemu ni ibada, ni heshima na kubwa zaidi husaidia wafiwa kuponya nafsi zao kwa kufunga ukurasa wa mpendwa wao wakibaki na matumaini kuwa wamempumzisha katika nyumba yake ya milele. 

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na WHO pamoja na shirika la chama cha Msalaba mwekundu ICRC na Mwezi mwekundu IFRC imeeleza kuwa miili ya watu ambao wamekufa kutokana na majeraha, katika majanga ya asili au vita kamwe haileti hatari ya kiafya kwa jamii. 

Hii ni kwa sababu watu hao ambao wamekufa kutokana na kiwewe, kuzama au moto hawahifadhi katika miili yao  vinavyosababisha magonjwa ambayo yatahitaji jamii kuchukua tahadhari za kawaida.

Dkt. Kazunobu Kojima ni Afisa Tiba wa ulinzi na usalama wa katika Mpango wa Dharura wa Afya wa WHO na ametoa ombi kwa mamlaka zote duniani. “Tunahimiza mamlaka katika jamii zilizoguswa na msiba kutoharakisha mazishi ya halaiki au kuchoma maiti. Usimamizi wenye heshima ni muhimu kwa familia na jamii, na katika maeneo yaliyo na migogoro, mara nyingi, ni sehemu muhimu ya kukomesha haraka mapigano.”

WHO imeeleza kuwa eneo ambalo kuna magonjwa kama Ebola, Marburg au kipindupindu, au wakati maafa mengine yanapotokea katika eneo lenye magonjwa hayo ya kuambukiza hapo ni vyema kuzika marehemu haraka kwani magonjwa ya mlipuko yanaweza kutokea.

Naye Mkuu wa kitengo cha uchunguzi wa ICRC Pierre Guyomarch amesema “Imani kwamba maiti yoyote itasababisha magonjwa ya mlipuko haiungwi mkono na ushahidi wowote” na kutoa wito kwa wanao elimisha jamii kuzingatia utoaji taarifa sahihi.

Tumekuwa tukiona ripoti nyingi za vyombo vya habari na hata wataalamu wakikosea katika kushughulikia suala hili, ukweli ni kwamba wale wanaookoka kwenye matukio kama msiba wa asili wana uwezekano mkubwa wa kueneza magonjwa kuliko maiti.” Amesema Guyomarch. 

Mashirika hayo kwa pamoja yamehimiza jamii kupatiwa zana na taarifa sahihi ili kupunguza hofu na ili waweze kudhibiti na kuhifadhi maiti kwa usalama na heshima. Na wale wanaohusika katika kushughulikia majanga wanapaswa kufuata kanuni zilizowekwa za usimamizi wa maiti, kwa manufaa ya jamii yote, na watoe msaada zaidi kama inahitajika.