Huduma inayofanywa na walinda amani wa Afrika iko katika fikra zetu-Antonio Guterres.

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki,  mjini Addis Ababa, Ethiopia katika picha hii ya kutoka maktaba
UN /Antonio Fiorente
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akiwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Moussa Faki, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika picha hii ya kutoka maktaba

Huduma inayofanywa na walinda amani wa Afrika iko katika fikra zetu-Antonio Guterres.

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezishukuru nchi wanachama wa Muungano wa Afrika na Kamisheni ya Muungano wa Afrika kwa kuunga mkono operesheni za amani barani Afrika akisema kuwa huduma na kujitolea kunakofanywa na walinda amani wa Afrika kuko katika fikra zetu. Guterres amesifu kazi inayofanywa na walinda amani ikiwa ni sehemu ya hotuba yake ya leo jumapili kwa wakuu wa nchi wanaokutana katika mkutano wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia.

Guterres amezungumza siku moja baada ya walinda amani watatu wa Ethiopia wanaohudumu katika shughuli za Umoja wa Mataifa katika eneo la Abyei mpakani mwa Sudan na Sudan Kusini (UNISFA) wamefariki katika ajali ya helikopta ya kijeshi iliyokuwa imebeba vikosi ilipoanguka ikiwa katika shughuli za kila siku. Abiria kumi wamejeruhiwa na ikiripotiwa kuwa watatu wako katika hali mbaya zaidi.

Akifafanua ukweli kuwa nchi za Afrika zinachangia takribani nusu ya walinda amani wote wakiwemo theluthi mbili ya walinda amani wanawake na sehemu kubwa wa polisi wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Guterres ameendelea mbele na kutambua kujitolea kwa askari wa kiafrika katika vikosi vya muungano nchini Somalia AMISOM na katika katika kikosi cha nchi tano G5 ambao wanapambana na ugaidi katika eneo la Sahel huko kaskazini mwa Afrika na pia vikosi vya nchi mbalimbali katika eneo la bonde la ziwa Chad vilivyowekwa ili kurejesha usalama katika eneo ambalo limeathiriwa na kundi la Boko Haram.

Tweet URL

 

Guterres amesema, "shughuli hizi za amani za Afrika zinahitaji mamlaka imara kutoka kwa Baraza la Usalama na ufadhili  endelevu wa kifedha, ikiwa ni pamoja na michango inayotathiminiwa."