Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili kutokomeza ukimwi ifikapo 2030 kila mtu lazima ajumuishwe hata watumia mihadarati: UNAIDS

Moldova inapanua huduma za kupunguza madhara kwa kuhakikishahuduma zizo zinafikia wafungwa magereza yote.
UNAIDS
Moldova inapanua huduma za kupunguza madhara kwa kuhakikishahuduma zizo zinafikia wafungwa magereza yote.

Ili kutokomeza ukimwi ifikapo 2030 kila mtu lazima ajumuishwe hata watumia mihadarati: UNAIDS

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na vita dhidi ya ukimwi UNAIDS limesema ili kuhakikisha ukimwi unatokomezwa ifikapo mwaka 2030 basi kila mtu anapaswa kujumuishwa katika vita hivyo ikiwemo wafungwa na wanaotumia mihadarati, kwani Mifumo mingi ya magereza inajitahidi kukabiliana na msongamano, rasilimali duni, ufikiaji mdogo wa huduma za afya na huduma zingine za msingi, vurugu na matumizi ya dawa za kulevya.

Nchini Moldova, gereza namba 16 la Pruncul moja ya magereza ambako UNAIDS inashirikiana na serikali na mamlaka za afya kuhakikisha wafungwa na hasa wanaotumia mihadarati wanapata huduma za kudhibiti virusi vya ukimwi au VVU na kukabiliana na athari za matumizi ya mihadarati.

Shirika hilo linasema mwaka 2021, idadi ya wafungwa magerezani duniani kote iliongezeka kwa asilimia 24 ikilinganishwa na mwaka wa 2020 hadi kufikia zaidi ya watu milioni 10.

Usambazaji wa methadone gerezani.
UNAIDS
Usambazaji wa methadone gerezani.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya Umoja wa Mataifa ya dawa za kulevya na uhalifu UNODC katika baadhi ya nchi hadi asilimia 50 ya watu walio gerezani hutumia au hujidunga dawa za kulevya ambayo ni moja ya sababu kubwa ya maambukizi ya magonjwa yatokanayo na damu kama vile VVU na hepatitis C.

Moldova ni miongoni mwa nchi zilizathirika na matatizo haya kwani tangu mwaka

2000, ni magereza machache tu nchini humo yaliyokuwa yakitoa huduma za kupunguza madhara. Lakini sasa kwa msaada wa UNAIDS magereza yote 17 yana huduma na mfungwa yeyote mpya katika jela za nchi hiyo anawajibika kumuona daktari wa magonjwa ya akili, na daktari wa kawaida kwa vipimo na ikihitajika basi anajumuishwa katika mpango wa matibabu.

Mfungwa Alexander Godin ni miongoni mwa waathirika anapitia katika milango kadhaa iliyofungwa katika gereza namba hili huku akisindikizwa na mlinzi hadi kwenye duka la dawa gerezani hapo. Hii ni sehemu ya utaratibu wake wa kila siku. Anakuja kuchukua dawa yake ya maji ya methadone baada ya kuacha uraibu wa dawa za kulevya, 

"Nimekuwa kwenye matibabu mbadala ya methadone kwa miaka 10. Familia yangu ilifanya uamuzi huu. Kabla ya hapo, nilitumia dawa za kulevya, afuni. Kwa hili, pesa zilihitajika, na hapo ndipo shida zilianza katika familia. Familia ilipendekeza niende kujiorodhesha kwenye zahanati inayotoa matibabu na tangu hapo nimekuwa kwenye mpango huo.”

Alexander Godin anapokea matibabu ili aweze kuondokana na matumizi ya madawa ya kulevya na methadone ambayo amezitumia kwa muda mrefu akiwa gerezani.
UNAIDS
Alexander Godin anapokea matibabu ili aweze kuondokana na matumizi ya madawa ya kulevya na methadone ambayo amezitumia kwa muda mrefu akiwa gerezani.

Methadone ni tiba inayosaidia watu kukabiliana na dalili za athari za mihadarati, msongo wa mawazo, kupunguza utegemezi wa heroini na kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwenye sindano zenye maambukizi.

Maria Potrimba, mkuu, idara ya magonjwa ya kuambukiza, Gereza hapa anasema "Ikiwa mgonjwa yuko kwenye matibabu haya mbadala, anafahamu zaidi kuhusu athari na anazingatia zaidi matibabu yake."

Maambukizi ya VVU ni asilimia 11 kati ya watu wanaojidunga dawa za kulevya nchini Moldova ambao ni zaidi ya asilimia 0.36 ya watu wote. Na ni moja ya makundi yaliyoathirika zaidi nchini humo.

Svetlana Plamadeala, ni mkurugenzi wa UNAIDS nchini Moldova amasema, 

"Nchini Moldova mzigo wa VVU ni mkubwa zaidi miongoni mwa makundi muhimu na pia huathiri wafungwa. Ofisi UNAIDS nchini humu iliunga mkono serikali kufanya majaribio ya programu za kupunguza madhara na matibabu ya mbadala wa afyuni magerezani tangu mapema mwaka wa 2000. Leo tunasherehekea ukweli kwamba tumepanua wigo wa huduma hizo kutoka kwenye mradi wa majaribio hadi kwenye mfumo mzima wa magereza au kila gereza lina huduma hizo. Ni katika kutoa kipaumbele kwa watu na pia ni kuhusu mtazamo wa afya ya umma.”

UNAIDS, na washirika wengine wa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu wamekuwa wakiunga mkono kupanua huduma hizi kwenye magereza yote.

Kwa sasa, kulingana na Harm Reduction International, ni nchi 59 pekee duniani ndio zinazotoa huduma hizo katika magereza yake.