Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatutovumilia uingiliaji wa msaada wa chakula tunachogawa Ethiopia:WFP

Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.
WFP Ethiopia
Msafara wa WFP ukiwa na msaada wa vyakula kwa ajili ya watu Tigray Ethiopia na Afar.

Hatutovumilia uingiliaji wa msaada wa chakula tunachogawa Ethiopia:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema  limesikitishwa sana na ripoti za hivi karibuni za kupelekwa kusikokusudiwa kwa idadi kubwa ya msaada wa kibinadamu wa chakula katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Shirika hilo limesema linalichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa na halitavumilia uingiliaji wowote katika usambazaji wake wa msaada muhimu wa chakula kwa wanawake, wanaume na watoto walio hatarini zaidi.

WFP imesema katika taarifa yake iliyotolea mjini Roma Italia kwamba mara moja imeanzisha uchunguzi wa kina baada ya kupata taarifa za mgao wa chakula kupelekwa kwingineko na imechukua hatua za haraka kubaini ukweli wote na kuimarisha udhibiti wa msaada wake zaidi.

“WFP imesitisha usambazaji wa chakula huko Tigray, ambao hautaanza tena hadi WFP ihakikishe kuwa msaada muhimu utawafikia walengwa wake.” Limesisitiza shirika hilo.

Tunashirikiana na serikali kuwabaini wahusika

WFP imesema  inafanya kazi kwa karibu na mamlaka za kikanda ili kubaini watu wowote wanaohusika katika shughuli hizi, na kuziba mianya yoyote katika mchakato wa kuwatambua na kuwasajili walengwa.

WFP pia inasisitiza kwa washirika wake kwamba wafuatile na kuripoti shughuli zozote zisizo halali, na kuwataka watekeleze udhibiti uliokubaliwa wa chakula cha msaada.

WFP inajivunia kuhakikisha matumizi sahihi ya michango ya wafadhili yenye udhibiti na michakato iliyoratibiwa zaidi ili kuwahudumia vyema mamilioni ya wenye njaa wanaotegemea msaada wa WFP wa kuokoa maisha na kubadilisha maisha.

Watu wa Tigray bado wanajikwamu kutokana na athari za vita vya miaka miwili ambavyo vimewaacha asilimia 84 ya watu katika ukanda huo kwenye mgogoro wa chakula.

Shirika hilo limesema limejizatoto kuhakikisha msaada wa chakula wa kuokoa Maisha unawafikia wale wanaouhitaji zaidi na kwa ufanisi.