Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makazi mapya kwa wakimbizi wa Kisomali yafunguliwa nchini Ethiopia:UNHCR

Wakimbizi wanendelea kuwasili Ethiopia baada ya kukimbia mapigano nchini Somalia.
© UNHCR/Muluken Tadesse
Wakimbizi wanendelea kuwasili Ethiopia baada ya kukimbia mapigano nchini Somalia.

Makazi mapya kwa wakimbizi wa Kisomali yafunguliwa nchini Ethiopia:UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, likionya kuhusu mgogoro unaoendelea Somalia ambao umesababisha watu kukimbia makazi yao na kwenda kusaka usalama nchini Ethiopia.

Uhamisho wa watu walio hatarini zaidi umeanza, limesema shirika la UNHCR, baada ya kuibuka kwa ghasia katika mji wa Lascanood kaskazini mwa Somalia na kusukuma karibu watu 100,000 kukimbilia eneo la mbali la jimbo la Somali nchini Ethiopia katika miezi miwili iliyopita.

Olga Sarrado, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
UN Geneva
Olga Sarrado, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

"Tangu mapigano yalipoanza katikati ya mwezi Februari, maelfu ya watu wamewasili katika eneo la Somali la Ethiopia kutafuta usalama. Kufikia wiki iliyopita, watu 91,000 walikuwa wamesajiliwa na mamlaka ya Ethiopia." Kwa mujibu wa msemaji wa UNHCR Olga Sarrado.

Bi. Sarrado ameongeza kuwa ingawa kasi ya kumiminika kwa walimbizi  wanaowasili jimboni Somali imepungua lakini wakimbizi hao wanaendelea kuwasili wakikimbia mashafuko Somalia.

Ethiopia hivi sasa inahifadhi jumla ya karibu wakimbizi 990,000 kutoka nchi jirani zikiwemo Sudan Kusini, Somalia, Eritrea na Sudan.

Maelfu ya watoto wawasili bila wazazi

Kulingana na UNHCR, wengi wa wakimbizi wanaowasili kutoka Somalia ni wanawake, watoto na wazee, wakiwemo "zaidi ya watoto 3,400 na vijana waliotenganishwa na wazazi au walezi na bila wa kuwasindikiza".

Bi. Sarrado amesema kwamba wakimbizi hao wameiambia UNHCR hadithi zenye kuhuzunisha za jinsi walivyotenganishwa na familia zao wakati mapigano yalipoanza na tangu wakati huo hawakuweza kufanya tena mawasiliano na jamaa na familia zao.

Kuhamisha walio hatarini zaidi

Sasa, UNHCR inasema uhamisho wa baadhi ya wakimbizi unaendelea, na watu 1,036 walio hatarini zaidi wamehamishwa kutoka maeneo ya mpakani hadi kwenye makazi mapya kwa muda wa siku tatu zilizopita".

Usafiri hadi kwenye kambi mpya, iliyo umbali wa kilomita 50 kutoka mpaka wa Mirqaan, wilaya ya Bokh, unaandaliwa na mamlaka ya Ethiopia pamoja na UNHCR na washirika wengine.

Maelfu ya wakimbizi wawasili Ethiopia, wakikimbia mapigano nchini Somalia.
© UNHCR/Nimo Ahmed Abdullahi
Maelfu ya wakimbizi wawasili Ethiopia, wakikimbia mapigano nchini Somalia.

Ulinzi na huduma bora

Bi. Sarrado amesema kuwa "Serikali ya Ethiopia imetenga kwa ukarimu ekari 400 ambapo wakimbizi wanaweza kukaa na kupata huduma zilizopo, kama vile huduma za afya, maji na elimu", na kuongeza kuwa "UNHCR inaendelea kushirikiana na mamlaka za mitaa na viongozi kutathmini mapungufu katika huduma za msingi, hivyo msaada unanufaisha wakimbizi na Waethiopia pia ambao ni wenyeji wao”.

Huku mahitaji yakiongezeka, uanzishwaji wa makazi mapya umefanyika kusaidia kuwapa wakimbizi wapya waliowasili ambao wamekuwa wakiishi katika mazingira hatarishi na makazi duni, msaada muhimu kama vile chakula na maji.

Bi. Sarrado ameeleza kuwa "uhamishaji wa watu hao unafanyika kwa sababu wakimbizi hao walikuwa wanakaa kwenye mpaka na Somalia, wakilala nje, na pia maeneo waliyokuwa wanakaa yalianza kuwa na msongamano mkubwa, na kusababisha kuongezeka kwa hatari za ulinzi".

Mgogoro wenye sura nyingi

Mapigano ya Lascanood, ambao ni mji mkuu wa eneo la Sool na sehemu ya eneo lililojitenga la Somaliland, ni ya kupinga wanajeshi wa Somaliland na ukoo wa eneo hilo kudai mji huo.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Mataifa na muungano wa washirika wa kimataifa walilaani ghasia hizo na kuelezea wasiwasi wao kuhusu mashambulizi dhidi ya raia, wakitoa wito wa "kufikiwa bila vikwazo vya kibinadamu katika eneo hilo ili kushughulikia kwa haraka mahitaji ya wale waliolazimika kuhama na kuathiriwa na vurugu zinazoendelea”.

Mwezi Machi, UNHCR na washirika wa kibinadamu walizindua mpango wa mashirika mbalimbali wa dharura wa dola milioni 116 ili kukabiliana na mahitaji muhimu yanayowakabili wakimbizi na jamii zinazowahifadhi katika eneo hilo.

Wiki iliyopita tu, katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu mzozo huo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema kuwa hali imeongezeka kuwa mbaya "wakati ambapo watu katika mkoa wa Sool wanakumbwa na uhaba wa maji usio na kifani kutokana na ukame mkali unaowakabili kuna hatari kubwa ya milipuko ya magonjwa."

Somalia na nchi jirani ya Ethiopia zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukame wa kihistoria wa miaka mitano mfululizo katika Pembe ya Afrika.