Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 445 zahitajika kukabiliana na maelfu ya watu wanaokimbia Sudan:UNHCR

Takriban watu 30,000 wamekimbilia Chad tangu mzozo uzuke Sudan, kwa mujibu wa UNHCR.
© UNHCR/Colin Delfosse
Takriban watu 30,000 wamekimbilia Chad tangu mzozo uzuke Sudan, kwa mujibu wa UNHCR.

Dola milioni 445 zahitajika kukabiliana na maelfu ya watu wanaokimbia Sudan:UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limesema linapanga kusaidia wakimbizi 860,000 na waliorejea kutoka Sudan na hivyo likishirikiana na wadau wengine, litahitaji dola milioni 445 kusaidia wakimbizi hao kuanzia sasa hadi mwezi Oktoba.

Ainisho hilo limewekwa kwenye muhtasari wa awali wa mpango wa kikanda wa hatua kwa wakimbizi wa Sudan, ambao umewasilishwa kwa wafadhili leo. Kimsingi fecha hizo zitashughulikia uungwaji mkono wa haraka wa msaada kwa wakimbizi nchini Chad, Sudan Kusini, Misri, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Mpango huo umeundwa na washirika 134 wakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali au NGOs za kitaifa na kimataifa na mashirika ya kiraia.

Hali ya kibinadamu ni mbayá

"Hali ya kibinadamu ndani na nje ya Sudan ni ya kusikitisha kuna uhaba wa chakula, maji na mafuta, upatikanaji mdogo wa usafiri, mawasiliano na umeme, na kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu," amesema Raouf Mazou, kamishna mkuu msaidizi wa operesheni wa UNHCR.

Ameongeza kuwa "UNHCR na washirika wana timu za dharura zilizopo na wanasaidia mamlaka kwa msaada wa kiufundi, kusajili wanaofika, kufanya ufuatiliaji wa ulinzi na kuimarisha mapokezi ili kuhakikisha mahitaji ya haraka yanatimizwa. Huu ni mwanzo tu. Msaada zaidi unahitajika haraka.”

UNHCR imekuwa ikiratibu mipango ya dharura na washirika kwa ajili ya watu wapya wanaowasili wakiwemo wakimbizi, wakimbizi wanaorejea na watu wengine katika nchi jirani.

Idadi yawatu 860,000 ni makadirio ya awali ya mipango ya kifedha na uendeshaji. Kati ya jumla, ya watu wapatao 580,000 ni Wasudan, wakimbizi 235,000 ni wale waliohifadhiwa hapo awali na Sudan wakirejea nyumbani katika hali mbaya, na wakimbizi wengine 45,000 ni wa mataifa mengine waliokuwa wakiishi Sudan hapo awali.

Misri na Sudan Kusini zinatarajiwa kushuhudia idadi kubwa zaidi ya watu wanaoingia wakikimbia machafuko Sudan.

UNHCR imekuwa ikiwapatia hifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko Sudan na kuingia Chad.
© UNHCR/Colin Delfosse
UNHCR imekuwa ikiwapatia hifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko Sudan na kuingia Chad.

Watu zaidi ya 330,000 wametawanywa

Kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi mapigano ya sasa tayari yamewatawanya zaidi ya watu 330,000 ndani ya Sudan huku zaidi ya wakimbizi wengine 100,000 na waliorejea wakiondoka nchini humo.

UNHCR leo imezindua mtandao wa takwimu ambao utaorodhesha idadi mpya ya kila siku ya wakimbizi na wanaorejea  na watu wanaowasili katika nchi jirani.

“Kuendelea kwa mapigano, uporaji, kupanda kwa gharama na ukosefu wa usafiri kunafanya iwe vigumu kwa watu kuondoka katika maeneo hatarishi huku upatikanaji wa huduma za afya pia ukiwa umeathiriwa sana” limeongeza shirika hilo.

Mpango huo utasaidia nchi wenyeji kuhakikisha upatikanaji wa hifadhi kwa wale wanaohitaji ulinzi wa kimataifa, kusaidia nchi mwenyeji kutoa msaada wa kuokoa maisha ya kibinadamu, kutambua walio hatarini zaidi na kuwapa huduma maalum. Kuwasili kwa msimu wa mvua kutaleta changamoto zaidi katika upatikanaji na utoaji wa misaada katika maeneo ya mbali.

Pia UNHCR inasema nchi nyingi zinazopokea wale wanaokimbia Sudan, na Sudan yenyewe, ni oparesheni ambazo tayari zilikuwa hazifadhiliwi kila wakati na zinapokea idadi kubwa ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao.

Na nyingi hadi sasa wamepokea chini ya asilimia 15 ya mahitaji ya ufadhili wanaouhitaji kwa mwaka  2023.

Mazou ameongeza kuwa "Tunahitaji ufadhili mpya kwa wakati unaofaa ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka. Mahitaji ni makubwa, na changamoto ni nyingi. Ikiwa mzozo utaendelea, amani na utulivu katika eneo lote vinaweza kuwa hatarini.”

Mpango wa kikanda wa kina zaidi wa hatua za kukabiliana na wakimbizi utazinduliwa wiki ijayo.