Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimekuja UN kuuonesha ulimwengu ni vitu gani vijana Tanzania tunafanya – Gibson Kawago

Gibson Kawago (katikati) akibadilishana mawazo na vijana wenzake wakati ya Jukwaa la Vijana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Aprili 2023, New York, USA.
UN
Gibson Kawago (katikati) akibadilishana mawazo na vijana wenzake wakati ya Jukwaa la Vijana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Aprili 2023, New York, USA.

Nimekuja UN kuuonesha ulimwengu ni vitu gani vijana Tanzania tunafanya – Gibson Kawago

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) la mwaka 2023 limeng’oa nanga jana tarehe 26 April ambapo maelfu ya viongozi vijana kutoka duniani kote wanakusanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kujadili pamoja na mambo mengine, masuala yanayolenga kuharakisha kujikwamua kutoka janga la COVID-19 na utekelezaji kamili wa Ajenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Jukwaa la Vijana ndilo jukwaa kuu la vijana kuchangia mijadala ya sera katika Umoja wa Mataifa, ambapo wanaweza kutoa maoni yao, wasiwasi wao, na kuzingatia suluhu zao za kibunifu ili kukabiliana na changamoto zinazokabili ulimwengu.

Mmoja wa vijana wanaohudhuria Jukwaa hili ni Gibson Kawago anayechakata betri chakavu za kompyuta na kuzirejesha katika matumizi mengine ya uzalishaji nishati. Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amezungumza na kijana huyu na swali la kwanza ni; umekuja na ujumbe gani kutoka Tanzania?

“Kwanza vijana wa Tanzania wanapambana sana.” Ndivyo anavyoanza Gibson Kawago na anaendelea akisema, “vijana wa Tanzania wanajitahidi sana kuja na suluhisho ambazo zitatua matatizo ambayo tofautitofauti katika jamii. Kwa hiyo mimi nimekuja kuwawakilisha na kuonesha ulimwengu ni vitu gani ambavyo Tanzania tunafanya.”

Gibson akitoa mfano wa kampuni yake inayofahamika kwa jina WAGA ambako wanachakata betri za kopyuta ambazo zimeharika na kuwatengenezea wananchi wa vijijini nishati mbadala anasema, “wanaweza kuchaji kwa kutumia umeme wa jua na kuweza kuangalia televisheni pamoja na kuchaji simu zao. Kwa hiyo nimekuja kuwaonesha kwamba sisi watanzania tumeanza kwa sehemu yetu tuungane kwa pamoja kwenda mbele zaidi.”

Kuhusu ni mambo gani mahususi ambayo wanayajadili katika Jukwaa hili la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) la mwaka 2023, Gibson anamjibu Flora Nducha akisema, “kitu kikubwa kabisa tulichokuwa tunazungumza ndani ni kuanzia kwenye upande wa será tulikuwa na baadhi ya wawakilishi kutoka nchi tofauti ambao wanahusika kwenye kutunga sera za nchi kuzungumza kuangalia ni sera zipi tunazihitaji ziweze kubadilishwa katika mifumo ambayo tunayo ili tuhakikishe sisi vijana vitu tunavyovifanya vinakuwa vimewekwa katika mfumo wa serikali pamoja na mifumo ya maisha yetu ya kila siku.”

Gibson Kawago akizungumza na Flora Nducha hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) la mwaka 2023.
UN News

Kubadilishana uzoefu

Gibson Kawago anasema amefurahi kukuta katika Jukwaa hili la Vijana kuna watu kutoka mataifa mbalimbali na hivyo vijana wamebadilishana uzoefu, “tulikuwa tunabadilishana kuona matatizo tofauti tunayokutana nayo kwa mfano sasa hivi mabadiliko ya tabianchi kuna upungufu wa mvua  unaona watu wamelima lakini mazao yanakufa, mifugo inakufa kwa sababu vyanzo vya maji vinakauka kwa hiyo tukawa tunazunguza kwamba nyinyi kwenu hili tatizo mnalitatua vipi? Na sisi tuangalie katika mazingira yetu tutakaporudi tutatatua vipi. Kwa hiyo ilikuwa ni muda wa kuongea, kuweza kubadilishana mawazo na kuweza kubadilishana mawazo na kuangalia kwa pamoja tutaungana vipi na tutakuja na kitu kimoja ambacho tutaweza kuweka malengo ya miaka inayofuata.”