Kifo cha bibi kilinichochea kusaka suluhu ya tatizo la umeme vijijini- Gibson

Katika karakana ya Gibson Kawago ambako wanarejelea betri chakavu za kompyuta mpakato ili kuzalisha makasha ya betri yanayotumika kupatia nishati ya umeme.
Gibson Kawago
Katika karakana ya Gibson Kawago ambako wanarejelea betri chakavu za kompyuta mpakato ili kuzalisha makasha ya betri yanayotumika kupatia nishati ya umeme.

Kifo cha bibi kilinichochea kusaka suluhu ya tatizo la umeme vijijini- Gibson

Tabianchi na mazingira

Kijana Gibson Kawago kutoka Tanzania ambaye ni miongoni mwa vijana 17 walioteuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa viongozi vijana wa kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs amesema atatumia kipindi cha miaka miwili cha nafasi hiyo kusongesha hatua kwa tabianchi ikiwemo kutumia ugunduzi wake kuchakata betri chakavu za kompyuta kutengeneza betri za kuzalisha umeme katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Nina furaha sana kuteuliwa na nitakuwa balozi mwema

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiwa Dar es salaam nchini Tanzania, Gibson amesema amepokea kwa furaha kubwa uteuzi huu akisema, “nina furaha kubwa sana kuweza kuteuliwa na Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wangu kwenye kutatua matatizo katika jamii hii ninayotoka.

Kijana huyu mwenye umri wa miaka 27 ambaye sasa anamiliki kampuni ya WAGA inayotengeneza betri hizo amesema anaamini kilichomfanya ateuliwe ni kazi yake ya kulinda mazingira na kubuni mbinu za nishati salama.

“Sisi tunajihusisha kuchakata betri za kompyuta mpakato, sasa hivi watu wakibadilisha betri kwenye kompyuta zao wanazitupa na zinachafua mazingira, na mara nyingi zikiingia kwenye udongo huleta madhara kwa afya ya binadamu,” amesema Gibson.

Betri hizo zikiisha umeme huchajiwa kwa sola

Wanachofanya WAGA ni kuchakata hizo betri na kutengeneza kasha la betri ambalo hutumiwa na wananchi wa vijijini kutumia kupata nishati mbadala na wanachaji kwa sola. Betri hiyo hutumika katika kuwasha taa na hata kuwasha televisheni.

Tweet URL

Kifo cha bibi yangu kilinichochea kutafuta jawabu la nishati

Gibson anasema chanzo cha yeye kujikuta kwenye ubunifu huo ni kifo cha bibi yake. “Kuna siku nikiwa kijijini nilikuwa natumia simu yangu kumuonesha bibi picha za  harusi. Katikati betri ikaisha na hatukuwa na umeme. Kesho yake nikasafiri umbali mrefu hadi mjini kupata betri.”

Anasema hata hivyo aliporejea nyumbani alikuta bibi yake amefariki dunia kwa kuwa hali yake ya kiafya haikuwa nzuri.

“Kwa hiyo wakati napata maumivu yale na kuwaza ni watu wangapi wanapata matatizo hayo nje nilipofika Dar es salaam wakati nasoma Chuo Kikuu cha Teknolojia ya Ufundi, DIT nikaanza kutafiti ni kwa vipi naweza kutengeneza betri inayohifadhi umeme,” amesema Gibson.

Amesema alisaka mafunzo kwenye mtandao na hatimaye akaweza kutambua jinsi ya kuchakata betri chakavu za kompyuta mpakato ili kuzalisha umeme.

Sasa betri zinawasha televisheni na taa vijijini

Kwa mujibu wa Gibson, anatengeneza makasha ya betri kutokana na betri chakavu za Lithium na Ion, na betri.

“Nimeweza kutengeneza betri kubwa ambazo inawezesha mtu wa kijijini kuweza kuwasha televisheni, kuwasha taa zake na kuweza kutumia na ikiisha anaweza kuchaji kwa nishati ya jua au sola.

Kifuatacho ni nini?

Gibson amesema kipindi cha miaka miwili cha nafasi hiyo ya kijana kiongozi wa kusongesha SDGS, atajitahidi kuwa balozi mzuri kuhakikisha vijana wenzake wanafahamu jinsi gani ya kutunza mazingira na wanajua ni jinsi gani watatafuta fursa tofauti kutatua matatizo katika jamii zao na kuhakikisha wanatunza mazingira yao.