Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutumie elimu ili kutokomeza mchango wa utumwa – UN

Webster, msanii wa kufokafoka kutoka Canada akiwasilisha onesho katika makumbusho ya Beaux-arts huko Quebec nchini Canada, kwenye ukuta kukiwa na michoro ya watumwa.
Mbaï-Hadji Mbaïrewaye
Webster, msanii wa kufokafoka kutoka Canada akiwasilisha onesho katika makumbusho ya Beaux-arts huko Quebec nchini Canada, kwenye ukuta kukiwa na michoro ya watumwa.

Tutumie elimu ili kutokomeza mchango wa utumwa – UN

Utamaduni na Elimu

Kuwakumbuka mamilioni ya waafrika waliouzwa utumwani kunasaidia kurejesha utu kwa watu ambao walipokwa utu wao bila huruma, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake wa kuadhimisha hii leo siku ya kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa utumwa na biashata ya utumwa kupitia bahari ya Atlantiki .

Amesema historia ya utumwa ni historia ya machungu na ukatili ambayo inaonesha ubinadamu ukiwa katika kiwango kibaya zaidi.

Historia yenye pande mbili

“Lakini pia ni historia ya ujasiri wa kipekee ikionesha jinsi binadamu – kuanzia watumwa wenyewe kupambana dhidi ya mazingira magumu na dhalili hadi kufikia harakati za waliotokomeza utumwa, watu ambao walizungumza dhidi ya uhalifu wa kikatili,” amesema Katibu Mkuu.

Ushirika wa uovu

Kwa zaidi ya miaka 400, waafrika zaidi ya milioni 13 walisafirishwa kiharamu kuvuka baharí ya Atlantiki katika kile ambacho Katibu Mkuu amekiita biashara ya kikatili ya utumwa.

Wanawake, wanaume na watoto waling’olewa kutoka kwenye familia na makazi yao; jamii zikatenganishwa, miili yao ikageuzwa bidhaa na wakapokwa utu wao.

Hali ya isiyotoweka kwenye fikra

“Kile ambacho biashara ya utumwa kuvuka Atlantiki imefanya kinatujia mara kwa mara kwenye fikra zetu hadi leo hii. Tunaweza kuunganihsa karne za ukoloni hadi ukosefu wa usawa unaokabili dunia leo hii,” amesema Katibu Mkuu.

“Na tunaweza kutambua taswira za kibaguzi zinazopatiwa umaarufu ili kuhalalisha biashara ya utumwa wakati huu ambapo chuki kutoka weupe wanaojiona bora zinaanza kuibuka tena,” ameongeza Katibu Mkuu.

Kumbukumbu ya biashara ya utumwa Stone Town, Zanzibar Tanzania
UN/Israa Hamad
Kumbukumbu ya biashara ya utumwa Stone Town, Zanzibar Tanzania

Bwana Guterres amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mtu kutokomeza mchango wa utumwa unaochochewa sasa kupitia ubaguzi wa rangi kwa kutumia silaha kali zaidi ambayo ni elimu – ambayo ndio maudhui ya siku hii inayoadhimiwa leo hii.

Tuungane dhidi ya ubaguzi wa rangi

“Kufundisha historia ya utumwa kunaweza kusaidia kuzuia kutokea tena kwa tukio la utumwa,” amesema Katibu Mkuu.

“Kwa kujifunza fikra na imani zilizowezesha utumwa kushamiri kwa karne kunaweza kufichua ubaguzi wa rangi wa zama zetu za sasa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “kwa kuheshimu waathirika wa utumwa, tunarejesha mikakati fulani ya utu kwa wale ambao walipokwa utu wao.”

Katibu Mkuu ametoa wito kwa watu kokote pale waliko kusimama kidete na pamoja dhidi ya ubaguzi wa rangi na kwa pamoja kujenga dunia ambamo kwayo kila mtu, kokote aliko anweza kuishi kwa uhuru, utu na haki za binadamu zikizingatiwa.

UN na maadhimisho ya kumbukizi

Umoja wa Mataifa ulikuwa na msururu wa matukio ya kuadhimisha siku hii.

Mathalani Jumatatu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilikuwa na mkutano ambapo mwanafalsafa kutoka Brazil ambaye pia ni mwanahabari, Djamila Ribeiro alihutubia.

Bi. Ribeiro amekuwa anatumia elimu kukabili ubaguzi dhidi ya wabrazili wenye asili ya Afrika, ikiwemo kupitia kitabu chake kilichopata mauzo makubwa kiitwacho ‘Little Anti-Racist Manual’ halikadhalika kupitia akaunti yake ya Instagram yenye wafuasi zaidi  ya milioni 1.