Zaidi ya watu milioni 40 bado ni waathirika wa utumwa duniani kote.

2 Disemba 2018

Shirika la kazi duniani, ILO, linasema utumwa bado ni tatizo kubwa linalowathiri zaidi ya watu milioni 40 duniani kote, watoto wakiwa ni robo ya idadi nzima pamoja na uwepo wa itifaki ya kuzuia hali hiyo ya kulazimishwa kufanya kazi iliyofikiwa mwaka 2016.

ILO imesema hayo leo tarehe pili desemba ambayo ni siku ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza utumwa ikiwa ni kutekeleza azimio lililowekwa na Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1951.

Siku hii ni fursa ya kukuza uelewa kuhusu tatizo hili la kidunia na kujikita katika kumaliza mifumo mipya ya utumwa kama vile usafirishaji haramu wa watu, ukatili wa kingono, mifumo mibaya ya utumikishaji watoto, ndoa za lazima na utumiaji wa watoto katika migogoro ya kivita.

Taarifa hiyo ya ILO inasema kazi nyingi wanazopewa watoto ni unyonyaji wa kiuchumi kinyume na mkataba wa kinataifa wa haki za watoto ambao unatambua haki ya watoto kulindwa dhidi ya unyonyaji wa kiuchumi na kutumikishwa katika kazi ambazo zinaweza kuhatarisha maisha yao au kuingilia masomo yao au kuwaumiza kiafya na kimwili, kiimani, kimaadili au maendeleo ya kijamii.

Usafirishaji haramu wa binadamu pia unazuiwa na itifaki ya kuzuia kukandamiza na kusafirisha watu kiharamu hasa wanawake na watoto. Hiyo ni kutokana na mkataba ulioidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2000, mkataba ambao unasema kuwa usafirishaji haramu wa watu ni kuwachukua watu, kuwasafirisha, kuwahamisha, au kuwapokea kwa mfumo wa kuwatisha au kutumia nguvu au aina nyingine ya matumizi ya nguvu kwa lengo la unyonyaji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud