Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hata kama tumetoboa masikio, hatujatobolewa akili, tuna uwezo wa kuleta maendeleo- Mary

Wanawake na wasichana wa kimasai katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
© UNICEF/UN0323295/Frank Dejongh
Wanawake na wasichana wa kimasai katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Hata kama tumetoboa masikio, hatujatobolewa akili, tuna uwezo wa kuleta maendeleo- Mary

Wanawake

Nchini Kenya, mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO wa ubia wa maendeleo kati ya sekta ya umma na binafsi, PPDP umewezesha wanawake wa jamii ya kimasai katika eneo la Rift Valley kujiinua kiuchumi na kijamii.

Mmoja wa wanufaika hao ni Mary Nkisonkoi kutoka kijiji cha Oloshaiki kilichoko eneo la Rift Valley au Bonde la Ufa nchini Kenya.

Mary kupitia chapisho na video ya ILO anasema alikuwa na bahati sana kuchaguliwa kuwa mwezeshaji wa jamii katika mradi wa PPDP.

“Kabla ya mradi huu kuanza, wanawake katika eneo letu hawakuwa wanakutana na kuzungumza kwa uwazi na kina matatizo na changamoto zinazowakabili. Hatukuruhusiwa kufanya hivyo labda pale tu ambapo waume zetu walifahamu kile ambacho kinajadiliwa,” anasema Mary.

Walikuwa wamezoea kusalia kijijini na kukutana kanisani na baada ya ibadi kila mtu anarejea nyumbani na kuendelea na wajibu wake wa kifamilia. Hatukufahamu kuwa sisi wanawake na akina mama tunaweza kufanya kitu na kusaidia kama jamii au kama wanawake.

PPDP ikabisha hodi Oloshaiki

Mradi wa PPDP ukaingia na ukaanza kufundisha wanawake kuhusu jinsia, haki za wanawake na tofauti kati ya mke na mume.

Hii ilituhamasisha kuzungumza na wanaume wetu,” anasema Mary huku akiongeza kwamba alifundishwa kuwa mwezeshaji ili kuwaleta pamoja wanawake na wanaume katika majukwaa ya umma. “Niliwaita wazee wa kijiji, wanawake, viongozi wa vikundi vya kijamii ili kujadili ni jambo gani lifanyike ili kuinua eneo letu.”

Mabadiliko chanya ya kujivunia

Mary anasema mabadiliko ya kwanza kutokea na ambayo anajivunia ni pale wanawake walipoweza kupata elimu ya watu wazima. “Tulifundishwa na mwalimu kutoka mradi wa PPDP. Tulifundishwa pia jinsi ya kuendesha biashara.”

Wanawake wengi walijiunga na darasa kwa sababu “hatukuwa na njia nyingine ya kujipatia kipato. Kwa asili, wanawake hawawezi kuuza ng’ombe au mahindi kwa sababu shamba ni mali ya mume.”

Walijipanga vema ili wasikose darasa

Mary anasema mwanzoni ilikuwa changamoto, lakini walijifunza kujipanga mapema kuhakikisha majukumu ya nyumbani na uchungaji wa mbuzi na ng’ombe unafanyika asubuhi. Ikifika saa 8 adhuhuri watoto wanaporejea nyumbani kutoka shuleni, wanawake walienda darasani.

“Wanawake walijifunza alfabeti pamoja nan amba na matokeo yake waliweza kutumia simu za rununu au za kiganjani,” anasema Mary.

Baada ya kujua kusoma na kuandika, nini kilifuatia?

Mwezashaji huyu wa jamii anasema baada ya darasa la elimu ya watu wazima, walifikiria ni nini tena wanaweza kufanya na kuleta mabadiliko zaidi.

“Tulianzisha kikundi cha upatu. Siku yetu ya soko ni jumatano ambako  wanawake wanauza maharage, viazi au mboga za majani. Tuliamua kukutana kila Alhamisi baada ya siku ya soko na kila mwanamke alete dola senti 40 au dola senti 81. Na iwapo mwanamke anataka kukopa fedha kukuza biashara yake, tunamkopesha na atarejesha na riba. Kisha tutampatia tena mwanamke mwingine akuze biashara yake.”

 Mafanikio mengine sasa wanaume wamepata uelewa wa kuwapatia wake zao nafasi na fursa kwa sababu Mary anasema, “nilipoketi nao kama mwezeshaji, niliwaeleza kuwa akina mama nao wanaweza kuleta kipato nyumbani, wakalipa karo na hata kununua chakula.”

Sasa anasema wako huru kuanzisha na kumiliki biashara. Kila mwanamke anaweza kupeleka kitu nyumbani na kuweka mezani, hata kiwe kidogo kiasi gani.

Hata shilingi 500 za Kenya saw ana dola 4.10. Tunawaambia waume zetu hiki ndicho nilichopata,” anasema Mary akiongeza kuwa hayo ni mabadiliko makubwa na hatuishi kama tulivyokuwa tunaishi zamani.

Mary anasema “ninajiambia katika biashara yangu siku moja nitakuwa miongoni mwa nyota zinazong’ara kwenye eneo hili.”

Kupitia ujasiriamali wa kukuza ng’ombe bora, Mary ameweza kujenga nyumba yake na anatamatisha akisema, “wanawake si watu wa kukandamizwa. Pale mwanamke anapoelimishwa, jamii itanufaika zaidi. Kwa hiyo nasihi wanawake waamke, wachukue nafasi za uongozi na kupigani hazi zao nchini Kenya.”