Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zama za taifa moja kutumia lugha moja na kuengua nyingine zimepitwa na wakati- Mtaalamu Huru

Bango la siku ya Lugha mama
UNESCO
Bango la siku ya Lugha mama

Zama za taifa moja kutumia lugha moja na kuengua nyingine zimepitwa na wakati- Mtaalamu Huru

Utamaduni na Elimu

Kuelekea siku ya kimataifa ya lugha ya mama duniani hapo kesho, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu makabila madogo amesema serikali lazima zichukue hatua zaidi juu ya matumizi ya lugha za makabila hayo madogo kwani zama za kuchagua lugha moja tu kutumiwa na taifa zima huku nyingine zikienguliwa zimepitwa na wakati.

Mtaalamu huyo Fernand de Varennes amenukuliwa kwenye taarifa iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR akisema lugha ni mbinu muhimu ya mawasiliano na kubadilishana ufahamu, kumbukumbuku na historia, lakini zaidi ya yote ni muhimu katika watu kuweza kuwasiliana kwa ukamilifu na kuweza kushiriki kwenye shughuli za taifa lao. 

Amesema ni kwa msingi huo, moja ya mbinu fanisi za kujengea uwezo makabili madogo na watu wa jamii ya asili ni kuwapatia hakikisho la kutumia lugha zao kwenye elimu, hususa kama lugha ya kufundishia, ali mradi inawezekana na vile vile lugha hiyo kuweza kutumika kutolea huduma za umma na fursa za ajira. 

Bwana de Varennes amesema “lugha pia ni haki ya msingi ya binadamu kwa makabila madogo na jamii ya watu wa asili na mimi na wataalamu wengine huru wa Umoja wa Mataifa tumekuwa tukikosoa hatua ya kupunguza na katika maeneo mengine kuengua matumizi ya ufundishaji kwa kutumia lugha za makabila madogo.” 

Amesema badala ya kupunguza au kuengua matumizi ya lugha hizo, serikali ziwekeze katika kuandaa zana za kufundishia, kufundisha walimu na kuendeleza matumizi ya lugha mama kwenye utoaji wa elimu pale inapowezekana ili kuhakikisha Watoto wa makabila madogo na jamii ya asili wanapata stadi za kusoma na kuandika zitakazowawezesha kujifunza lugha zingine ikiwemo lugha rasmi. 

Mtaalamu huyo amesema hiyo ndio njia fanisi ya kuhakikikisha usawa na kutokoweko na ubaguzi na kuheshimu sheria ya kimataifa. 

Amesema uteuzi wa lugha moja tu kutumika kila mahali na kuengua zingine ni kinyume na ujumuishi wa jamii na kwamba siku ya kimataifa ya lugha ya mama na muongo wa kimataiffa wa lugha ya jamii ya asili ni fursa za kusongesha na kufurahia utajiri wa lugha na tamaduni mbalimbali duniani. 

Siku ya lugha ya mama huadhimiwa tarehe 21 ya mwezi Februari kila mwaka.