Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndani ya siku mbili ahadi kwa ‘Elimu Haiwezi Kusubiri’ zafikia zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 826  

Yabanziri, mama wa watoto wawili, aliweza kurejea shuleni kwa msaada kutoka ECW katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Vittoria Moretti
Yabanziri, mama wa watoto wawili, aliweza kurejea shuleni kwa msaada kutoka ECW katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ndani ya siku mbili ahadi kwa ‘Elimu Haiwezi Kusubiri’ zafikia zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 826  

Utamaduni na Elimu

Viongozi wa dunia wametangaza zaidi ya dola za Marekani milioni 826 kwa Education Cannot Wait (ECW) au Elimu Haiwezi Kusubiri ambao ni mfuko wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa elimu katika dharura na migogoro ya muda mrefu. 

Mkutano huu wa sasa wa ngazi za juu ulikuwa unalenga kutafuta ufadhili wa kusaidia elimu ya wasichana na wavulana milioni 222 wanaoishi katika maeneo yenye dharura kama majanga na pia mizozo. 

Taarifa hizi muhimu za ahadi ya dola milioni 826 zimetolewa katika Mkutano wa Ufadhili wa Ngazi ya Juu wa ECW leo tarehe 17 Februari huko Geneva, Uswisi ikiwa ni hatua muhimu katika kutimiza ahadi ya kimataifa ya kutoa elimu kwa wote ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. 

Kwa ujumla, wafadhili 17 wametangaza ahadi zao kwa ‘Elimu Haiwezi Kusubiri’, ikijumuisha michango mitano kutoka kwa wafadhili wapya ambayo ni hatua ya kihistoria ya mpango wa Elimu haiwezi Kusubiri na elimu katika dharura na migogoro ya muda mrefu.  

Mwezi mmoja kufikia Mpango Mkakati mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa mwaka 2023-2026, ahadi hizi muhimu tayari zinafikia zaidi ya nusu ya dola za Marekani bilioni 1.5 zinazohitajika kutekeleza Mfuko wa Mpango Mkakati wa miaka minne na kufikia watoto na vijana milioni 20. 

Pamoja na vita nchini Ukraine, kutokuwa na uhakika wa kiuchumi duniani na rekodi kubwa ya watu kulazimika kuyahama makazi yao na mizozo ya kibinadamu inayoharibu mafanikio ya maendeleo kote Afrika, Asia, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini, ahadi hizo mpya zinaashiria dhamira muhimu ya kimataifa ya kuweka ufadhili wa elimu katika dharura na kwa migogoro ya muda mrefu katika kilele cha ajenda ya kimataifa. 

Duniani kote, watoto milioni 222 walioathiriwa na migogoro, mabadiliko ya tabianchi, kulazimishwa kuhama makazi yao na migogoro mingine ya muda mrefu wanahitaji haraka elimu bora. Pamoja na washirika wake, ECW inaongoza njia ya kuwafikia wasichana na wavulana hawa kwa usalama, matumaini na fursa ambayo elimu iliyokamilika pekee inaweza kutoa. 

Ignazio Cassis wa Bunge la Shirikisho la Uswisi amenukuliwa akisema, “hakuna demokrasia bila elimu. Ni lazima tuweze kutegemea vizazi vijavyo vilivyoelimika vyema. Amani, uhuru na ustawi wa mataifa yote unategemea hilo.”  

Uswisi ni mwenyeji wa Mkutano huu wa Ngazi ya Juu wa Ufadhili ikishirikiana na ECW na Serikali za Colombia, Ujerumani, Niger, Norway na Sudan Kusini. Kupitia ushirikiano wa kiubunifu na sekta ya kibinafsi, benki ya Zürcher Kantonalbank  chini ya wawekezaji wa ziada  imejitolea kusimamia kituo ambacho kinaweza kuhamasisha ufadhili endelevu na unaotabirika kwa ECW, mfuko wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa elimu katika dharura na migogoro ya muda mrefu. 

Ujerumani inasalia kuwa mfadhili mkuu wa ECW  

“Watoto wengi sana, hasa wa kike, hawana fursa ya kupata elimu bora ya kuwapatia nyenzo za maisha bora ya baadaye, njia ya kutoka katika mzunguko wa umaskini na kukata tamaa. Hatuwezi kumudu kupoteza kizazi hiki. Ahadi za leo zitasaidia kuwapa mamilioni ya vijana walio hatarini zaidi matumaini. Ujerumani tayari ilitangaza mwaka jana kwamba tutaunga mkono Mpango Mkakati wa kuwasaidia watoto hawa kwa euro milioni 210 kwa miaka minne ijayo. Leo, tulijumuika na wafadhili wengine wengi. Kwa pamoja, tumebeba jukumu letu la pamoja. Lakini kuwa wazi: juhudi zetu za pamoja haziwezi na hazitaishia hapa.” Amesema Svenja Schulze, Waziri wa Shirikisho wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo, Ujerumani. 

Uingereza nayo 

Uingereza imetoa ahadi kubwa zaidi mpya kwa siku hii, ikitangaza ufadhili mpya wa pauni milioni 80 kwa ECW. Kwa mchango huu muhimu, Uingereza inaendelea kuwa wafadhili wa pili kwa ukubwa wa ECW. 

"Nimerejea kutoka Niger ambako niliona jinsi elimu inavyobadilisha maisha ya vijana ambao wanafurushwa na migogoro na uhaba wa chakula. Kuelimisha watoto na vijana walioathiriwa na migogoro ni mojawapo ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo - kuanzia uvamizi haramu wa Urusi nchini Ukraine hadi tetemeko la ardhi lililoharibu hivi majuzi huko Uturuki na Syria na bila kusahau kizazi cha wasichana waliopigwa marufuku kikatili kuhudhuria shule nchini Afghanistan. Tunaiweka tena dhamira yetu ya elimu katika dharura kwa sababu tunakataa kukata tamaa kwa watoto na vijana milioni 222 walioathiriwa na vitisho vya vita, maafa na kufurushwa. Elimu inaweza kutoa suluhu kwa maisha bora ya baadaye.” Amesema Waziri wa Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo Andrew Mitchell. 

Canada imetangaza Dola milioni 87.5 za Canada (CAD $ 87.5) katika ufadhili mpya wakati wa kikao cha juu cha ahadi. 

Washirika wapya ambao wamejiunga na orodha inayokua ya wafadhili wa ECW katika Kongamano la Ufadhili wa Ngazi ya Juu, kwa michango ya mara ya kwanza kutoka kwa Muungano wa Biashara wa Kimataifa ni Italia, Qatar, Uhispania na Zürcher Kantonalbank. 

Michango kutoka kwa wafadhili na usaidizi mpana kutoka kwa serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa, sekta ya kibinafsi, mashirika ya kiraia na washirika wengine wa kimkakati wanaanzisha harakati za kimataifa za kubadilisha utoaji wa elimu kwa watoto walioathiriwa na matatizo na kuchochea uwekezaji zaidi ili kutoa msaada wa elimu kamilifu duniani kote. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Education Cannot Wait Yasmine Sherif akihitimisha kikao cha ngazi ya juu cha amewashukuru wafadhili kwa michango yao na kutoa wito kwa viongozi wa dunia kuongeza ufadhili wa Elimu.