Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa "Elimu haiwezi kusubiri" waonesha mafanikio makubwa katika kuwapatia elimu wasichana na wavulana walio katika maeneo ya mizozo

Wasichana katika shule ya Jean Vcolmomb huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.
©Education Cannot Wait
Wasichana katika shule ya Jean Vcolmomb huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mradi wa "Elimu haiwezi kusubiri" waonesha mafanikio makubwa katika kuwapatia elimu wasichana na wavulana walio katika maeneo ya mizozo

Utamaduni na Elimu

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Elimu Haiwezi kusubiri Education Cannot Wait (ECW), ambao ni mfuko wa kimataifa wa elimu katika maeneo ya dharura na migogoro ya muda mrefu, umetoa Ripoti yake ya Mwaka ya Matokeo, ambayo imefichua kuwa licha ya msukosuko wa kimataifa, mfuko huo na washirika wake wameendelea kupanua wigo wao wa utoaji msaada. 

Hali ilivyo mpaka sasa

Ripoti hiyo iliyosomwa hii leo 23 Agosti 2022 inaonesha kuwa uwekezaji wa ECW umefikia karibu watoto na vijana milioni 7 sawa na asilimia 48.4 kati yao wakiwa wasichana  tangu kuanza kazi mwaka 2017.

Aidha, kati ya watoto wote waliofikiwa na uwekezaji wa ECW hadi sasa, nusu ni wasichana, na asilimia 43 ni watoto wakimbizi au wakimbizi wa ndani.

Mwaka 2021, ECW ilifikia wanafunzi milioni 3.7 katika nchi 32 zilizokumbwa na majanga, asilimia 48.9 walikuwa wasichana. Wanafunzi wengine milioni 11.8 walifikiwa kupitia programu za mfuko wa fedha za  COVID-19. Miradi hii imetoa usaidizi kwa idadi ya watoto na vijana wanaosaidiwa na mfuko wa afua ya COVID-19 kufikia milioni 31.2, asilimia 52 wakiwa wasichana.

Yasmine Sherif, Mkurugenzi wa Elimu Haiwezi Kusubiri, akitoa tafakari juu ya maendeleo yaliyofikiwa na mfuko huo alisema “Matokeo madhubuti ya ECW katika miaka mitano ya kwanza ya kazi yetu ni uthibitisho wa dhana kwamba tunaweza kubadili mkondo na kuwawezesha wasichana na wavulana waliotengwa zaidi katika mizozo, kuwapa matumaini, ulinzi na fursa ya elimu bora.”

Watoto wakimbizi wa ndani wanahudhuria darasa katika shule moja nchini Cameroon.
© Education Cannot Wait/Daniel Beloumou
Watoto wakimbizi wa ndani wanahudhuria darasa katika shule moja nchini Cameroon.

Kazi imefanyika lakini safari bado ndefu

Matokeo ya ripoti hiyo yalitolewa kufuatia makadirio mapya ya kushtua yaliyotolewa na ECW mwezi Juni 2022, ambayo yalifichua kuwa duniani kote, wanafunzi milioni 222 wanahitaji msaada wa haraka wa elimu. Hii inajumuisha milioni 78.2 ambao hawajasoma na milioni 119.6 walio shuleni lakini hawajafikia umahiri wa chini kabisa katika masomo ya hisabati na kusoma.

"Wakati maendeleo yanaendelea kufanyika, bado tuna safari ndefu," alisema Gordon Brown, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Elimu ya Ulimwenguni.

Mkutano wa ngazi za juu wa ufadhili wa mradi huu wa 'Education Cannot Wait's utafanyika Geneva Uswisi mwezi Februari 2023. Utaandaliwa na nchi ya Uswisi wakishirikiana na ECW na kuitishwa kwa pamoja na Ujerumani, Niger, Norway na Sudan Kusini kupitia kauli kampeni yao ya Ndoto ya Milioni 222. Mkutano huo utatoa wito kwa watu binafsi na taasisi, katika sekta ya kibinafsi na ya umma, kutoa michango ya kifedha kwa ECW.

Sherif alisema, "tunaziomba serikali, wafanyabiashara, na watendaji wa hisani kutoa michango mikubwa ya ufadhili kwa ECW ili kusaidia kugeuza ndoto kuwa ukweli kwa watoto walioachwa nyuma zaidi katika mizozo."

Watoto kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wakihudhuria darasa katika eneo lililopatiwa ulinzi kwenye kambi ya wakimbizi nchini Cameroon.
© UNICEF/Sebastian Rich
Watoto kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wakihudhuria darasa katika eneo lililopatiwa ulinzi kwenye kambi ya wakimbizi nchini Cameroon.

Hatua zaidi zinahitajika

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mizozo, kulazimishwa kuyahama makazi yao, majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na athari za janga la COVID-19 zimechochea ongezeko la dharura za elimu. 
Fedha za ufadhili zilizoombwa zilifikia dola bilioni 2.9 mwaka 2021, ikilinganishwa na dola bilioni 1.4 mwaka wa 2020. Wakati 2021 ilishuhudia kuongezeka kwa ruzuku ya elimu ya dola milioni 645  nakisi ya jumla ya ufadhili iliongezeka kwa asilimia 17.
Kuendelea kuongezeka kwa upungufu wa ufadhili inaashiria mwelekeo unaotia wasiwasi wa uhaba wa rasilimali.