Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 222 walio katika maeneo yaliyoathirika na migogoro wanahitaji msaada wa haraka wa elimu:ECW 

Mtoto akitabasamu darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway kwenye maeneo nufaika ya miradi ya elimu inayofadhiliwa na pande mbili hizo.
ECW
Mtoto akitabasamu darasani wakati wa ziara ya pamoja ya ECW na Norway kwenye maeneo nufaika ya miradi ya elimu inayofadhiliwa na pande mbili hizo.

Watoto milioni 222 walio katika maeneo yaliyoathirika na migogoro wanahitaji msaada wa haraka wa elimu:ECW 

Utamaduni na Elimu

Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaohusika na kusongesha elimu kwenye maeneo yenye majanga na mizozo ya muda mrefu, Education Cannot Wait, ECW au kwa lugha ya Kiswahili, Elimu Haiwezi Kusubiri, pamoja na wadau wamesisitiza umuhimu wa kusaidia mamilioni ya watoto walio katika mazingira ya migogoro ili waweze kupata elimu, wakisema elimu ndio ufunguo wa kuwakomboa watoto hao hususan wasichana katika maisha yao ya siku za usoni.

Akizungumza katika mikutano mbalimbali ya ngazi ya juu hii leo mjini Dublin Ireland ikihusisha wawakilishi wa serikali na wadau wengine wa kimataifa wa elimu Yasmine Sherif mkurugenzi wa Education Cannot Wait, ECW au elimu haiwezi kusubiri amesema “Hivi sasa watoto na barubaru milioni 222 walio katika maeneo ayliyoathirika na migogoro wanahitaji haraka msaada wa elimu na zaidi ya nusu yao ni wasichana. Ni muhimu sana mfuko wa elimu haiwezi kusubiri kufandiliwa kikamilifu ili kuhakikisha wadau wetu wa kimataifa kama Plan International wanaweza kuendelea na kazi yao nyeti ya kutoa usalama, matumaini na fursa za elimu kwa wasichana na wavula walio katika hali mbaya zaidi duniani.” 

Bi. Sherif amesema ufadhili huo wa elimu uitasaidia kutimiza malengo ya ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu ikiwemo ahadi ya elimu kwa wote. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kimataifa wa Plan International Stephen Omollo, aliyeambatana na Bi. Sherif katika mikutano hiyo ameongezea kuwa
“Kwenda shule ni njia ya ukombozi wa maisha kwa watoto, hasa wasichana. Hata hivyo, duniani kote, watoto wananyimwa haki hii ya msingi. Tumesikia kuhusu kukaribia kupigwa marufuku kwa elimu ya wasichana nchini Afghanistan na matokeo mabaya ya hili. Lakini kunyimwa haki ya msingi ya elimu kwa wasichana kunakwenda mbali zaidi ya Afghanistan. Kuanzia Ukraine hadi Sudan Kusini, migogoro inavuruga elimu ya wasichana huku familia zikilazimika kukimbilia usalama wao na hakika, nusu ya watoto wote wakimbizi hawako shuleni, nahii si haki.” 

Yasmine Sherif Mkurugenzi wa Elimu haiwezi Kusubiri (ECW)  alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya mfuko wa elimu haiwezi Kusubiri (Kutoka maktaba)
ECW
Yasmine Sherif Mkurugenzi wa Elimu haiwezi Kusubiri (ECW) alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya mfuko wa elimu haiwezi Kusubiri (Kutoka maktaba)

Ameendelea kusema kuwa katika nchi nyingi elimu imekatizwa kutokana na njaa au mabadiliko ya tabianchi au wakati mwingine mchanganyiko wa mjanga yote hayo.

“Na wasichana wanapolazimika kuacha shule sio tu elimu yao na fursa zao zinazoathirika hususan kwa wasichana vigori wanakuwa katika hatari ya ukatili, manyanyaso, mimba za utotoni na mila zingine potofu za kikatili  kuanzia ndoa za utotoni hadi ukeketaji. "

Wadau hao wa elimu wameeleza kuwa migogoro, mabadiuliko ya tabianchi na majanga mengine vimeongeza mara tatu idadi ya watoto na vijana barubaru wanaohitaji msaada wa elimu kutoka milioni 75 mwaka 2015 hadi kufimia milioni 222 mwaka huu. 

Kwa mantiki hiyo wamesisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa ikiwemo Ireland kusaidia kufadhili mfumo huo wa elimu haiwezi kusubiri kwenye mkutano wa ufadhili wa elimu haiwezi kusubiri utakaofanyika Geneva Uswis mwaka huu kuanzi Februari 16-17.