Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na wadau wasaka dola milioni 605 kwa ajili ya wakimbizi wa DRC

Jimmy Ogwang, Afisa wa mashinani wa UNHCR eneo la Kisoro, akisaidia wakimbizi wapya kutoka DRC waliowasili katika kituo cha Bunagana ili waelekee kituo cha mpito cha Nyakabanda, kilichoko Kisoro nchini Uganda.
© UNHCR/Esther Ruth Mbabazi
Jimmy Ogwang, Afisa wa mashinani wa UNHCR eneo la Kisoro, akisaidia wakimbizi wapya kutoka DRC waliowasili katika kituo cha Bunagana ili waelekee kituo cha mpito cha Nyakabanda, kilichoko Kisoro nchini Uganda.

UNHCR na wadau wasaka dola milioni 605 kwa ajili ya wakimbizi wa DRC

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na mashirika 69 ya kiutu leo wametangaza ombi la dola milioni 605 kwa ajili ya kusaidia wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliosaka hifadhi kwenye nchi jirani za kusini na ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika. 

Msemaji wa UNHCR Olga Sarrado Mur amewaambia waandishi wa habari kuwa fedha hizo ni kwa mwaka huu wa 2023 na zitalenga pia jamii za wenyeji zinazowapatia hifadhi. 

UNHCR inasema hatua ya leo inatambua kuwa DRC inaendelea kukumbwa na janga la muda mrefu zaidi la kibinadamu barani Afrika, na kwamba zaidi ya wakimbizi na wasaka hifadhi milioni 1 kutoka taifa hilo wamekimbilia nchi jirani. 

Wakimbizi kutoka DRC wakisafirishwa kwa gari kwenda makazi ya wakimbizi ya Kyangwali huko Hoima nchini Uganda.
UN/John Kibego
Wakimbizi kutoka DRC wakisafirishwa kwa gari kwenda makazi ya wakimbizi ya Kyangwali huko Hoima nchini Uganda.

Uganda inaongoza kwa kuhifadhi wakimbizi wengi wa DRC Afrika 

Mathalani Uganda wako 479,400, Burundi 87,500, Tanzania 80,000, Rwanda 72,200, Zambia 52,100, Jamhuri ya Congo 28,600 na Angola 23,200. 

“Uganda inasaliwa kuwa taifa la Afrika linalohifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kutoka DRC. Mwaka 2022 pekee mashambulizi yanayofanywa na waasi mashariki mwa DRC yalisababisha wakimbizi 98,000 wakimbizi nchi yao ambapo nusu yao wako Uganda,” amesema Bi. Mur. 

Makazi na kambi za wakimbizi katika nchi zinazohifadhi wakimbizi zimefurika na huduma za kijamii kama vile afya, maji na huduma za kujisafi zimezidiwa uwezo au gharama zake ni kubwa. 

Uhakika wa kupata chakula nao unasuasua huku watu wakihaha kujikimu kutokana na ongeeko la bei za vyakula unaohusishwa na mzozo unaoendelea nchini Ukraine. 

Wahisani onesheni mshikamano na wanaohifadhi wakimbizi 

UNHCR na wadau wanatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuhakikisha wanaendelea kuonesha ukarimu wao kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi kutoka DRC, ili wakimbizi walio hatarini zaidi waweze kupatiwa huduma za ulinzi, chakula, afya, elimu na nyinginezo. 

“Pamoja na misaada ya dharura, ombi hili la 2023 linasaka kuongeza uwezo wa wakimbizi na jamii wenyeji kujitegemea na kuwa na mnepo,” amesema Bi. Mur akiongeza kuwa ombi litajikita zaidi katika harakati zinazoongozwa na wanawake na vijana ili hatimaye waondokane na utegemezi wa misaada. 

Hali tete ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ikichochewa na madhara ya muda mrefu ya janga la coronavirus">COVID-19 na ukosefu wa usalama kutokana na mashambulio ya vikundi vilivyojihami visivyo ya kiserikali pamoja na mapigano ya kikabila na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vinazuia fursa ya wakimbizi wa ndani kurejea nyumbani na katika shughuli zao za kujipatia kipato. 

“Vichocheo hivi vinataraijwa kuendelea kusababisha wakimbizi kukimbilia nchi jirani mwaka huu wa 2023,” amesisitiza msemaji huyo wa UNHCR. 

Ndani ya DRC hali ilivyo 

Ndani ya DRC pekee, nako zaidi ya watu milioni 5.8, wanawake, wanaume, wavulana, wasichana na watoto ni wakimbizi wa ndani kutokana na mizozo. 

Katika majimbo yaliyo mashariki mwa taifa hilo, zaidi ya vikundi 132 vilivyojihami ambavyo si vya kiserikali vinaendesha mashambulizi huku wakimbizi wengi wa ndani wakisaka hifadhi kwenye shule, makasani, mabohahi na kwa wenyeji. 

Tangu mwezi Machi mwaka jana wa 2022, takribani watu 521,000 wamekimbia jimbo la Kivu Kaskazini pekee.