Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 78 duniani kote hawaendi shule! Ajabu yastaajabisha na UN yataka hatua za haraka

Wanafunzi wawili wadogo huko Bol, Chad wakionyesha kazi yao kwenye ubao mweusi shuleni.
UNICEF/Frank Dejongh
Wanafunzi wawili wadogo huko Bol, Chad wakionyesha kazi yao kwenye ubao mweusi shuleni.

Watoto milioni 78 duniani kote hawaendi shule! Ajabu yastaajabisha na UN yataka hatua za haraka

Utamaduni na Elimu

Watoto wa kike na wa kiume milioni 78 duniani kote hawaendi shuleni kabisa kutokana na mapigano, mizozo, majanga ya tabianchi na ukimbizi ilhali wengine makumi ya mamilioni wanapata elimu ya hapa na pale, ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo huko Geneva, Uswisi. 

Akihutubia kwa njia ya video mkutano wa kusaka dola milioni 222 kusaidia elimu kwa watoto walio kwenye majanga na mizozo ulioandaliwa na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusongesha elimu kwenye maeneo ya majanga na mizozo ya muda mrefu, Education Cannot Wait au elimu haiwezi kusubiri, Katibu Mkuu amesema hakuna mtu anapaswa kunyimwa fursa ya kujifunza. 

Amesema kwa ujumla watoto milioni 222 million leo hii wanapata elimu isiyo na umakini. 

Msichana mdogo akiwa darasani nchini Yemen, ambapo mpango unaofadhiliwa na ECW unasaidia waalimu na wanafunzi katika upatikanaji wa elimu bora.
© Building Foundation for Development Yemen
Msichana mdogo akiwa darasani nchini Yemen, ambapo mpango unaofadhiliwa na ECW unasaidia waalimu na wanafunzi katika upatikanaji wa elimu bora.

Elimu ni haki ya msingi 

“Haijalishi uko wapi, haijalishi unaishi wapi na wala vikwazo unavyokumbana navyo, ni lazima upate elimu bora,” amesema Katibu Mkuu akitoa wito wa juhudi zaidi za kimataifa kuhakikisha watoto wengi zaidi walio hatarini na wengineo wanapata fursa ya kufanikiwa. 

Katibu Mkuu amekaribisha suala kwamba tangu mfuko huo uliopoanzishwa mwaka 2017, walimu 87,000 wamepatiwa mafunzo na kupatia watoto milioni 7 wanaoishi kwenye maeneo ya majanga elimu wanayostahili. 

Wakati ahadi kutoka nchi 18 na sekta binafsi zimefikia milioni 826 katika siku hii ya kwanza ya mkutano, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu Duniani na pia Mwenyekiti wa jopo la ngazi ya juu la ECW, Gordon Brown amekaribisha usaidizi wa kimataifa juu ya fursa ya kusoma kwa wote akisema ni uwekezaji wa amani endelevu. 

 “Tunazungumzia kuhusu watoto walio pembezoni zaidi, walio hohehahe na waliosahaulika zaidi duniani. Tunazungumzia kuhusu watoto wa kike ambao wanajikuta wakisafirishwa kiharamu au wakitumikishwa kwenye ajira au kulazimishwa kuolewa iwapo hatutawasaidia,” amesema Bwana Brown. 

Fedha zipelekwe pia kwa nchi zinazopokea wakimbizi- Bi. Lugangira 

 

Tweet URL

“Fedha zinazochangishwa hapa zipelekwe pia kwa nchi zinazopokea wakimbizi ili ziweze kutoa huduma inayotakiwa,” amesema Neema Lugangira, mbunge kutoka nchini Tanzania ambaye pia ni mwakilishi wa Afrika katika mtandao wa wabunge vinara wa elimu duniani. 

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutoka Geneva, Uswisi kunakofanyika mkutano huo, Bi. Lugangira amesema “jambo kubwa lazima kusisitiza ni kwamba mara nyingi inapofanyika michango ya fedha kama hizo, unakuta nchi ambazo zinapokea wakimbizi na kuwapatia huduma mbali mbali huwa zinasahaulika. Kwa hiyo nikiwa natoka Tanzania na kwa niaba ya mataifa mengine ya Afrika niko hapa kusisitiza umuhimu wa kukumbuka nchi kama Tanzania ili ziweze kuendelea kutoa misaada mbalimbali lakini ziweze kuwa nyumbani kwa wenzetu wanapopata changamoto mbalimbali.” 

Afghanistan: Kuhaha kupata vitabu vya kiada 

Akiwa na simulizi yake mwenyewe ya machungu kuhusu janga la elimu Afghanistan, Somaya Faruqi ameeleza washiriki kuwa alipokimbia nchi yake wakati watalibani walipotwaa mamlaka mwezi Agosti mwaka 2021, ndugu zake wengi wa kike walisalia nyuma. 

Hivi sasa marafiki wake wa kike hawawezi kusoma baada ya marufuku kutoka mamlaka zilizojitangaza za watalibani, amesema Faruqi mwenye umri wa miaka 20, ambaye bado anaendelea kuwasiliana nao na anafanya kazi kama mwanarahakati wa haki za wanawake ili kupaza majanga yao. 

“Hali ni mbaya kuliko uonavyo kwenye taarifa za habari,” ameileza Idhaa ya Umoja wa Mataifa. “Kila siku ninapokea ujumbe kutoka kwa marafiki zangu kwamba wanaozwa bila kujali umri au ridhaa yao. 

Wajibu mzito 

Ameongeza kuwa anahisi ana wajibu mkubwa kusaidia dada zake ambao bado wako Afghanistan. Kila siku nawasiliana nao hata kama hali zao si nzuri. 

“Nasikiliza simulizi zao, nawapatia maneno ya kuwatia moyo na kusaidia kuwaunganisha na rasilimali au vitu wanavyohitaji iwapo nina uwezo. Inavunja moyo kuona mapito yao, lakini hiyo inatia ari zaidi ya kusaka suluhu ya haki za wasichana na kusaidia kujenga mustakabali bora kwa wanawake wa Afghanistan."