Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imeongeza asilimia 43 ya mgao wa chakula kwa wakimbizi Rwanda

Mwanamke akitembea kwenye kijiji cha Kageyo kilichoko mashariki mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
WFP/Riccardo Gangale
Mwanamke akitembea kwenye kijiji cha Kageyo kilichoko mashariki mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

WFP imeongeza asilimia 43 ya mgao wa chakula kwa wakimbizi Rwanda

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani, WFP limeongeza kwa asilimia 43 mgao wa chakula kwa wakimbizi wanaoishi kwenye kambi zote tano nchini humo ili waweze kukidhi mahitaji yao ya msingi, kufuatia ongezeko la bei za vyakula na nishati duniani kote.   

Kuanzia mwezi huu wakimbizi walio hatarini zaidi watapokea dola 9 kwa mwezi kila mmoja kutoka dola 6, ilihali walio katika hatari kidogo watapata dola 4 kwa mwezi kila mmoja kutoka dola 3.  

Kwa mujibu wa WFP hizi ni mgao uliopunguzwa kutoka mgao wanaostahili ambao ulirekebishwa wa karibu dola 13 kwa wakimbizi walio katika hatari kubwa na karibu dola 8 kwa wakimbizi walio katika mazingira magumu kiasi kutokana na upungufu wa ufadhili wa WFP

Kupanda kwa gharama za maisha 

“Ufuatiliaji wa bei wa kila mwezi wa WFP unaonyesha kuwa wastani wa gharama za kikapu cha chakula kwa mwezi Desemba 2022 ulikuwa asilimia 77 zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa Desemba 2021 hali ambayo inawasukuma wakimbizi zaidi kwenye njaa,” anasema Ahmareen Karim, kaimu mkurugenzi wa WFP nchini Rwanda.  

Ameongeza kuwa "Usaidizi huu ulioongezeka utawapa wakimbizi chaguo zaidi kushughulikia mahitaji yao muhimu katika masoko ya ndani, na pia kusaidia kukuza uchumi wa ndani." 

Mwezi Mei 2021, WFP ilianzisha usaidizi unaotegemea mahitaji kwa wakimbizi nchini Rwanda ili kuhakikisha kuwa rasilimali chache zinapewa kipaumbele kwa wakimbizi walio hatarini zaidi.  

Kwa sasa, kati ya wakimbizi 127,000 wanaohifadhiwa nchini Rwanda, WFP inatoa msaada wa chakula na lishe kwa wakimbizi 113,650 walio katika kambi, huku asilimia 87 ya wakimbizi wote wakitajwa kuwa hatarini zaidi na asilimia 6 kuwa katika mazingira magumu kiasi.  

Watoto wachanga na watoto wadogo, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, watu wanaoishi na VVU na kifua kikuu hupokea msaada wa ziada wa lishe ili kuzuia na kutibu utapiamlo.  

Watoto wa shule kutoka jumuiya za wakimbizi na watoto kutoka jumuiya zinazowapokea wanaosoma shule zilezile pia hupokea uji wenye lishe kila siku au milo wa moto. 

Mwanamke akisafisha shamba lake mashariki mwa Rwanda ambapo shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP unawasaidia wakulima wadogo.
WFP/Rein Skullerud
Mwanamke akisafisha shamba lake mashariki mwa Rwanda ambapo shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP unawasaidia wakulima wadogo.

Ushirikiano na serikali na wadau 

WFP inafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Rwanda, washirika wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia kuchangia uhakika wa chakula wa makundi ya watu walio katika mazingira magumu, kama vile wakimbizi na wasaka hifadhi, licha ya ongezeko kubwa la bei ya chakula nchini kote. 

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi nchini humo UNHCR Aissatou Masseck Dieng-Ndiaye anatoa maoni akisema "Ongezeko la thamani ya msaada wa chakula kwa wakimbizi linakuja wakati muhimu. Mfumuko wa bei ukiwemo wa bei za vyakula, unafanya kuwa vigumu kwa wakimbizi kukidhi mahitaji yao ya msingi. Kwa kufanya kazi kwa karibu na WFP kubaini idadi ya wakimbizi walio hatarini zaidi, UNHCR inatumai kuwa mabadiliko haya ya hivi punde yatawazuia wakimbizi kutumia mikakati mibaya ya kukabiliana na hali hiyo na kuwasaidia kuzisaidia familia zao vyema zaidi.” 

Ongezeko la wakimbizi kutoka DRC 

WFP kwa sasa inaunga mkono miminiko la hivi karibuni wa wakimbizi wapya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa msaada wa chakula wa kuokoa maisha katika kambi ya mpito ya Nkamira. 

"Serikali ya Rwanda itaendelea kufanya kazi na washirika na washikadau wengine ili kuhakikisha ustawi na ulinzi kamili wa wakimbizi waliohifadhiwa na wanaotafuta hifadhi. Serikali pia itaendelea kuhakikisha kwamba jitihada na ahadi zake zote za ulinzi na ushirikishwaji wa wakimbizi zinatimizwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na sheria za kitaifa,” amesema Philippe Habinshuti, katibu mkuu katika wizara inayoshughulikia menejimenti ya dharura nchini Rwanda.