Skip to main content

 Mkimbizi kutoka Sudan apata kimbilio Rwanda baada ya madhila Libya 

Machwewo kwenye hifadhi ya taifa ya Nyungwe nchini Rwanda
Picha na WMO/Cyril Ndegeya
Machwewo kwenye hifadhi ya taifa ya Nyungwe nchini Rwanda

 Mkimbizi kutoka Sudan apata kimbilio Rwanda baada ya madhila Libya 

Wahamiaji na Wakimbizi

Takriban wakimbizi 2,500 na wasaka hifadhi wanashikiliwa katika vizuizi nchini Libya kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Muungano wa Afrika AU. 

Huyo ni mmoja wa wakimbizi hao Mohamed Daood Ali kutoka Sudan, katika video ya UNHCR mkimbizi huyo anaonekana kuwa na mawazo chungu nzima, yeye ni mmoja wa wakimbizi waliosafirishwa hadi Rwanda na baada ya kugundua kwamba yuko salama aliipigia simu familia yake kuwahakikishia usalama wake.

Kijana Ali kwa kipindi cha miaka miwili alipokuwa kizuizini nchini Libya alikuwa hajazunugmza na mama yake. Aliondoka Darfur, Sudan kwa matumaini ya kuvuka bahari ya Mediterranea na kuingia Ulaya lakini ndoto hiyo hakuwahi kuifikia na badala yake alijikuta katika mazingira magumu na hata ya manyanyaso na kudhalilishwa.

“Wakati unaniita mtumwa, hilo linaniuma zaidi ya kunipiga ngumi, hilo lazima unalijua, wakati mtu akikwambia kwamba wewe ni mtumwa…afadhali ujaribu kuniua lakini sio kuniita mtumwa, ninajua mimi ni nani.”

Mohamed alikuwa amepanga safari yake kupitia Libya kwa sababu alisikia kwamba watu hutumia njia hiyo kuvuka hadi Ulaya lakini alikabiliwa suluba.

“Walitupiga, watu wanasema kwamba sisi ni watumwa, wanapiga watu, kuwatesa na hakuna chakula.”

Lakini kama walivyonena wahenga hakuna lililo na mwanzo lisilokuwa na mwisho na madhilia yaliyomkuta Mohamed yalifika ukomo pale UNHCR ilipoanza kuwahamisha mamia ya wakimbizi na wasaka hifadhi kutoka Libya hadi Rwanda kuanzia Septemba mwaka huu wa 2019 ambapo baada ya kuwasili huko Mohamed anasema.

“Wakati nilikuja hapa, ninajihisi kuwa huru kwa sababu nchi hii ni tofauti, ninahisi kama nimerejea nyumbani, ndio hapa ni nyumbani kwangu. Ninahisi kwamba niko nyumbani wakati ninaona kwenye macho ya wanyarwanda wanapenda watu, ninaona upendo kwenye macho yako na ndio maana napenda nchi hii, napenda watu hawa.”

Kabla ya kufunga safari hiyo ya hatari, Mohamed alikuwa mwanafunzi wakati alipokimbia mzozo Sudan Magharibi.

Watu wanojaribu kuingia Libya bila kibali wako katika hatari ya kukamatwa na kuzuiliwa.