Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gabon, Jamaica na Sri Lanka zaungana kukabili vipodozi hatarishi kwa Ngozi

WHO imebaini zebaki kama moja ya kemikali 10 zinazoweza kuhatarish afya
WHO
WHO imebaini zebaki kama moja ya kemikali 10 zinazoweza kuhatarish afya

Gabon, Jamaica na Sri Lanka zaungana kukabili vipodozi hatarishi kwa Ngozi

Afya
  • Gabon, Jamaica na Sri Lanka wameunganisha juhudi zao kupunguza madhara ya kiafya na mazingira yasababishwayo na sekta ya vipodozi vya kuchubua Ngozi.
  • Mradi wa dola milioni 14  utasaidia mpango wa kutokomeza matumizi ya zebaki kwenye bidhaa za vipodozi na kupazia sauti urembo wa Ngozi za rangi zote.
  • Vipodozi vingi vya kuchubua Ngozi kuwa nyeupe vina madini ya zebaki, na kutishia afya ya binadamu na mazingira

Serikali za Gabon, Jamaica na Sri Lanka wamezindua mradi wa kutokomeza matumizi ya madini ya zebaki kwenye vipodozi vya kuchubua Ngozi kuwa nyeupe.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kulinda mazingira, UNEP iliyotolewa jijini Geneva, Uswisi hii leo imesema kitendo cha kutumia vipodozi vya kuzuia mwili kuzalisha melanin, ni tabia ya karne nyingi zilizopita katika sehemu mbali mbali duniani na inaendelea kusababisha janga hadi leo hii.

Melanin ni kemikali inayozalishwa na mwili ili kuepusha mwili kukumbwa na miali mikali ya  jua.

“Wanawake na wanaume wanatumia bidhaa za kujichubua, sio tu kwa ajili ya kufanya Ngozi yao iwe nyeupe bali pia kwa ajili ya kufifisha madoa usoni ikiwemo ya uzee na pia kuondoa chunusi,”  imesema taarifa hiyo ya UNEP.

Hata hivyo UNEP inasema mara nyingi watumiaji wanakuwa hawana uelewa ya kwamba bidhaa hizo zina kemikali  hatarishi kama vile zebaki, kemikali yenye sumu ambayo inahatarisha afya ya binadamu na pia chafuzi kwa mazingira.

Fahamu madhara ya kutumia bidhaa za kuchubua ngozi

Kwa mujibu wa UNEP, mafuta ya kuchubua ngozi iwe nyeupe yanaweza kusababisha:

  1. Vipele kwenye ngozi na mabaka mabaka kwenye ngozi ya rangi tofauti tofauti.
  2. Kuharibu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na mfumo wa kinga mwilini.
  3. Mtumiaji kukumbwa na kiwewe na msongo wa akili

Mkataba wa kimataifa wa Minamata kuhusu matumizi ya zebaki umeweka kiwango cha miligramu 1 ya zebaki kwa kila kilogramu 1 ya vipodozi vya kuchubua ngozi iwe nyeupe.

Hata hivyo Kikosi kazi cha kutokomeza zebaki na Taasisi ya Utafiti wa Bayonuai, mwaka 2018 walitafiti bidhaa 300 kutoka nchi 22 na kubaini kuwa asilimia 10 ya mafuta ya kuchubua ngozi iwe nyeupe yalivuka kiwango kilichopangwa cha zebaki mara 100 zaidi ya kiwango kinachotakiwa.

Mradi wa kutokomeza zebaki kwenye vipodozi

Sasa Gabon, Jamaica na Sri Lanka kwa pamoja wamezindua mradi wa dola milioni 14 utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mradi unaongozwa na UNEP huku fedha zikitolewa na Fuko la Mazingira Duniani, GEF na kutekelezwa kwa pamoja shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO na Taasisi ya Utafiti wa Bayonuai, BRI,

Mradi utalenga kupunguza hatari ya kupunguza vipodozi vyenye zebaki, kuelimisha umma juu ya madhara ya matumizi ya vipodozi hivyo, kutunga kanuni za kupunguza usambazaji wake, kukomesha uzalishaji, biashara na usambazaji katika masoko ya kitaifa na kimataifa.

Ni kwa vipi mtoto anaweza kudhurika na zebaki kwa kunyonya maziwa ya mama?

UNEP inasema bidhaa hizo za kuchubua Ngozi hazihatarishi afya ya mtumiaji pekee, bali pia watoto nao wanaweza kudhurika kwa kunyonya maziwa ya mama alyetumia mafuta hayo, halikadhalika kupitia mnyororo wa usambazaji vyakula kwani vyakula vinaweza kupata chembechembe za zebaki pindi vipodozi vinapotupwa kwenye majitaka.

Halikadhalika, kemikali hizo zinaweza kutiririka na kusalia kwenye maji au udongo.

“Mahitaji ya bidhaa hizo yakikadiriwa kuongezeka hadi thamani ya dola bilioni 11.8 mwaka 2026 kutokana na kukua kwa daraja la kati kwenye ukanda wa Asia- Pasifiki na kubadilika kwa mienendo ya makundi na uhitaji Afrika na Karibea, suala la matumizi ya kemikali hatarishi kwenye vipodozi vya kuchubua ngozi, ni jambo linalokuwa la kimataifa.”

Mkurugenzi wa Idara ya Viwanda na Uchumi UNEP, Sheila Aggarwal-Khan amesema matumizi ya vipodozi vyenye zebaki ni suala kubwa kwenye afya ya umma na linapaswa kushughulikiwa.

“Ingawa serikali zimekubali kuweka kiwango cha matumizi kupitia Mkataba wa Minamata, kampuni zinaendelea kuzalisha na kuuza vipodozi hatarishi,” amesema Bi. Aggarwal-Khan huku akisema UNEP inajivunia kufanya kazi na mataifa hayo matatu na wadau wengine ili kuleta mbadiliko kwenye sekta hiyo ya vipodozi.”