Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNITAID na mipango ya kudhibiti saratani ya shingo ya kizazi katika nchi za kipato cha chini

Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.
© UNICEF/Laurent Rusanganwa
Msichana mdogo nchini Rwanda akipokea chanjo yake ya HPV wakati wanafunzi wenzake wakisubiri zamu yao kwa woga.

UNITAID na mipango ya kudhibiti saratani ya shingo ya kizazi katika nchi za kipato cha chini

Afya

Tarehe 4 Februari ni Siku ya Saratani Duniani ambayo mwaka huu inalenga kuongeza uelewa na kuhamasisha hatua za kuziba pengo la huduma za kuudhibiti ugonjwa huu hatari.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID linatahadharisha kuwa uhaba wa upatikanaji wa huduma za kinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi unawafanya mamilioni ya wanawake hasa katika nchi zenye uchumi mdogo kuwa hatarini na ndio maana shirika hilo na wadau wake wameandaa na kutekeleza mpango madhubuti wa zana na mikakati inayokidhi mahitaji ya huduma za afya ya kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi.

Tenu Avafia, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID anasema “Saratani ya shingo ya kizazi inazuilika sana wakati wanawake wanapopata huduma ya uchunguzi wa mapema na matibabu. Changamoto ni kwamba, katika mazingira ya watu wa kipato cha chini, ambapo upatikanaji wa huduma hizi ni nadra, viwango vya saratani ya shingo ya kizazi ni karibu mara mbili ya ilivyo katika nchi zenye kipato cha juu. Mbaya zaidi, tunaona kwamba vifo tisa kati ya kumi vinavyotokana na saratani ya shingo ya kizazi hutokea miongoni mwa wanawake katika mazingira ya kipato cha chini.” 

UNITAID na wadau wake wameunda na kutekeleza mpango wa kifurushi cha zana na mikakati ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi ambayo inakidhi mahitaji ya huduma za afya katika nchi hizi hasa katika hatua za mwanzo za kuchunguza na kudhibiti virusi vifahamikavyo kama Human Papilloma au kifupi HPV ambavyo vinahusishwa moja kwa moja na saratani ya shingo ya kizazi. 

Nchi ambazo ziko katika mradi huu wa UNITAID ni Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Malawi, Nigeria, Ufilipino, Rwanda na Senegal na tayari yanatumia kifurushi hiki cha zana kuvuka lengo la shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO la ifikapo mwaka 2030 kutokomeza ugonjwa huu wa saratani ya shingo ya kizazi kwa kutibu asilimia 90 ya wanawake wote wanagundulika kuwa na vidonda vya kabla ya saratani. Tenu Avafia Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Unitaid anarejea tena kufafanua vizuri kuhusu hilo akisema, "UNITAID inafanya kazi na wadau wake kuendeleza kifurushi cha zana ambazo zimechukuliwa kulingana na mahitaji ya afya ya nchi hizi. Mipango yetu katika nchi 7 tayari inaonesha kwamba inawezekana kufikia malengo ya WHO kwa ajili ya kutokomeza saratani ya shingo ya kizazi katika mazingira ya kipato cha chini. Na, kama tungeongeza hatua hizi, tungesaidia kuepusha kuendelea kwa saratani kwa wanawake duniani kote. 

Vipimo vipya vya HPV vinaziba pengo la njia isiyo sahihi sana ya uchunguzi wa kutumia macho kukagua shingo ya kizazi. UNITAID inasema zaidi ya asilimia 50 ya wanawake waliofikiwa kupitia programu hizo katika nchi 7 wamefanyiwa uchunguzi wa HPV hadi kufikia sasa. 

Vifaa ambavyo vinatumia betri na kushilikiwa kwa mkono vinaruhusu matibabu ya haraka ya vidonda vya kabla ya saratani katika vituo vya afya vya msingi. Vifaa hivyo huchukua nafasi ya vyombo vizito vya matibabu na hivi vipya vinapunguza muda wa matibabu kufikia dakika moja hadi mbili, ikilinganishwa na 15. 

Antoinette Mukamwiza, ni Muuguzi katika Kituo cha Afya cha Remera mjini Kigali Rwanda, ni shuhuda wa ufanisi wa vifaa hivi vipya vilivyoletwa na UNITAID na wadau wake,“upimaji huu ni wa siri. Wanawake hujihisi huru wanapojipima wenyewe, na hii inasaidia katika kuharakisha kazi yetu kwa sababu wanawake wawili au watatu wanaweza kujipima kwa wakati mimi nikiendelea na kufanya usajili. Inanisaidia kupokea wagonjwa wengi kwa muda mfupi.” 

Makubaliano ya bei yaliyopatikana kupitia uwekezaji wa UNITAID yamepunguza gharama ya uchunguzi wa HPV kwa theluthi moja na kupunguza bei ya vifaa vya kukausha vidonda kwa joto, na kufanya matibabu kuwa chini mara kumi kuliko matibabu ya kutumia ile njia ambayo kitaalamu inaitwa cryotherapy kwa maana ya kutumia baridi kali katika eneo lililoathirika. 

UNITAID inasisitiza kuwa njia hizi za kukinga kwa kutambua na kutibu shingo ya kizazi kabla ya saratani zinaunganishwa katika miundo iliyopo ya afya ili kuongeza chanjo na ufahamu. Yakitekelezwa kwa upana, suluhu hizi zinaweza kufikia lengo la WHO la matibabu ya kabla ya saratani na kuchangia kuepusha karibu vifo milioni 65 vinavyotokana na saratani ya shingo ya kizazi katika karne ijayo.