Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azolla, gugu maji liligeuka mkombozi kwa wakulima, wafugaji na vijana Tanzania

Ben Lyimo, mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania akilisha magugu maji aina ya Azolla kwa ng'ombe mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania.
UN News
Ben Lyimo, mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania akilisha magugu maji aina ya Azolla kwa ng'ombe mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania.

Azolla, gugu maji liligeuka mkombozi kwa wakulima, wafugaji na vijana Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Azolla ambao ni mmea aina ya magugu maji, umeanza kupata umaarufu duniani kutokana na uzalishaji wake wa kasi, ukitumia eneo dogo, halikadhali kwa kuwa ni lishe bora kwa mifugo kama vile ng’ombe na kuku.

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO linasema Azolla ina kiwango kikubwa cha protini ghafi kuanzia asilimia 19 hadi 30, ikilinganishwa na mazao mengi ya kijani kibichi pamoja na yale yameayo kwenye maji.

Azolla na ufanikishaji wa SDGs

Ni kwa mantiki hiyo gugu maji hilo linaonekana linaweza kuchangia katika kufanikisha lengo namba 1 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs la kupunguza umaskini.

Nchini Tanzania, tayari wafugaji wa ng’ombe na kuku, wamejikita kwenye uzalishaji wake, halikadhalika vijana wanaoona ni fursa ya kuwawezesha kujipatia kipato.

Wafugaji Kigoma nao wanafahamu

Kupitia Mradi wa Pamoja wa Kigoma, KJP nchini Tanzania unaotekelezwa na  mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la chakula na kilimo, FAO,  Selemani Munisi, mtaalamu wa mifugo toka Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma anafahamu jinsi ya umuhimu wa Azolla kwenye mifugo.

“Tunatumia Azolla au gugumaji kama kirutubisho kwenye chakula cha kuku,” anasema Bwana Munisi.

Upandaji wa Azolla

Akiwa mbele ya shamba hilo la Azolla, mtaalamu huyu anasema la muhimu kwanza ni kuchimba shimo lisilozidi futi moja na kisha kutanguliza karatasi la nailoni na kisha kuweka maji. “Karatasi la nailoni linazuia maji kufyonzwa na ardhi kwa kuwa mmea  huu unahitaji maji muda wote. Kisha  unapanda miche ambapo ni kuchuka tu kiasi cha magugu maji hayo na kuweka kwenye kidimbwi cha maji.”

Kidimbwi cha kupanda gugu maji aina ya Azolla.
UN News
Kidimbwi cha kupanda gugu maji aina ya Azolla.

Mavuno ni siku tatu tu

Alipoulizwa ni muda gani unahitajika kuvuna Azolla, anasema ni siku tatu tu inakuwa imekamilika kuvunwa na kupatiwa mifugo kama kuku, ng’ombe na nguruwe.

« Nasihi wafugaji watumie sana Azolla kwa licha ya kwamba ni kirutubisho, pia kinapunguza gharama ya chakula cha kuku ambacho ni bei ya juu, » amesema Bwana Munisi.

Vijana wameitikia wito

Mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania kwenye Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, SUA, mwanafunzi wa mwaka wa pili  wa shahada ya Sayansi, Ben Lyimo ametambua umuhimu wa Azolla katika sio tu kulinda mazingira bali pia kumwongezea kipato kwa sababu yeye hakupata mkopo wa masomo kutoka serikali.

Yeye ameomba kiambaza cha eneo alilopanga chumba kuweka dimbwi la kupanda Azolla ambazo huuzia wateja wake takribani dola 6 kwa kilo.

« Ujuzi wa kilimo cha Azolla nimepata kupitia mitandao ambako naona watu wanafanya nini na pia ninasoma tafiti mbalimbali, » anasema Ben akiongeza kuwa kupitia mauzo ya Azolla ameweza kujenga mtandao na watu wengi na zaidi ya yote anapata kipato cha kujikimu mahitaji yake.

Azolla pia inalinda mazingira

Mwanafunzi huyu anaendelea kusema kuwa anajikita kwenye kilimo kutekeleza pia sera za kitaifa na kimataifa, mathalani kitaifa ya kutaka vijana kutumia fursa zilizopo kujenga uchumi kwa njia bora. « Kimataifa nalinda mazingira. »

FAO inasema kuwa Azolla ambayo imekuwa inatumiwa muda mrefu barani Asia ni mbolea isiyoharibu mazingira kwa ajili ya mazao badala ya kutumia zile za kemikali.